Katibu Mkuu wa Hezbollah Seyyed Hassan Nasrallah |
Katibu Mkuu wa kundi la Hezbollah, Seyyed Hassan Nasrallah anasema kuwa marafiki wa Syria hawatakubali kuiona Damascus ikiangukia mikononi mwa Marekani, Israel, na waasi wanaoendesha harakati zao katika taifa hilo la Kiarabu.
“Syria ina marafiki wa kweli katika ukanda huu na duniani kwa ujumla ambao hawataiacha Syria iangukie mikononi mwa Marekani, Israeli au makundi pinzani; hawatakubali hilo litokee," alisema Nasrallah katika hotuba yake iliyorushwa na vituo vya televisheni mjini Beirut Lebano jana Jumanne.
Aliongeza kuwa juhudi zinazofanywa na Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu, zinazowaunga mkono waasi nchini Syria, zinalenga kuiondoa nchi hiyo katika nafasi ya kuwa mhimili wa mapambano dhidi ya Israeli katika ukanda huo.
“Unaweza kusema kwa dhati kabisa kuwa lengo la wale walio nyuma ya machafuko ya Syria ni kuliangamiza taifa la Syria, watu wa Syria, jamii na jeshi ili Syria igeuke kuwa taifa lililoshindwa ambalo haliwezi kufanya uamuzi kuhusu mafuta, gesi na rasilimali zake," alisema.
Mkuu huyo wa Hezbollah alisema kuwa hatua ya mgogoro huo kuendelea kwa muda wa miaka miwili inaashiria kuwa serikali ya Damascus haiwezi kuangushwa kupitia njia za kijeshi.
Aidha, Nasrallah alisema kuwa “ufumbuzi na suluhu ya kisiasa kwa ajili ya hali ya Syria" ndiyo njia pekee inayoweza kuutatua mzozo wa sasa nchini humo.
Syria imekuwa katika mzozo mbaya sana tangu mwezi Machi 2011, na watu wengi wamepoteza maisha yao.
Serikali ya Syria inadai kuwa mzozo huo unachochewa kutoka nje ya nchi hiyo, huku kukiwa na ripoti kuwa wapiganaji wengi wanaopigana dhidi ya serikali wanatoka nje ya Syria.
0 comments:
Post a Comment