Askari wa Ufaransa katika operesheni ya kijeshi kwenye mtaa mmoja katika mji wa Gao, nchini Mali Aprili 13, 2013. |
WAZIRI wa ulinzi wa Ufaransa amethibitisha kwamba wanajeshi wake 1000 waliopo nchini Mali wataendelea kubaki huko kupambana na makundi yenye silaha hata baada ya kuwasili kwa walinda amani 12,000 wa Umoja wa Mataifa baadaye mwaka huu.
Siku moja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha matumizi ya kikosi cha kulinda amani, Waziri wa ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian alifanya ziara katika mji wa Gao kaskazini mwa Mali.
“Kuanzia sasa tupo katika awamu ya baada ya vita. Azimio la Umoja wa Mataifa lililotangazwa jana litaruhusu ujio wa kikosi kitakachoweka uthabiti katika nchi hii," Le Drian aliwaambia waandishi wa habari hapo jana Ijumaa. “Lakini Ufaransa itawabakisha askari wake 1000 kuendelea na operesheni za kijeshi."
Wakati wa zaiara yake hiyo, Le Drian alikutana na Rais wa mpito, Dioncounda Traoré na Jenerali Ibrahim Dahrou Dembele kujadili juhudi za mpango wa kutoa mafunzo kwa jeshi la Mali.
Aidha, kikosi cha Umoja wa Mataifa kitajumuisha askari 6000 wa Umoja wa Afrika walioko Mali - kikosi ambacho hivi karibuni afisa mmoja wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani alikiita kuwa ni kikosi "kisichojiweza kiabisa".
Kikosi cha Umoja wa Mataifa kitakuwa na jukumu la kusaidia kurejesha amani baada ya operesheni ya kijeshi iliyonzishwa na Ufaransa mwezi Januari kwa lengo la kupambana na wapiganaji waliokuwa wamelidhibiti eneo kubwa la kaskazini mwa nchi hiyo.
Hata hivyo, walinda amani wa Umoja wa Mataifa hawataruhusiwa kuanzisha operesheni za kijeshi au kufukuzana na waasi katika jangwa. Hivyo, askari wa Ufaransa wataendelea kufanya kazi hiyo, japokuwa Ufaransa yenyewe inapanga kupunguza kikosi chake katika koloni lake hilo la zamani ifikapo mwisho wa mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment