Kiongozi wa Kanisa azikwa akiwa hai mkoani Mbeya


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani

Msaidizi wa zamani wa Padri (Katekisita) katika Kigango cha Kanisa Katoliki Kijiji cha Mkwajuni, Florian Mwamosi (70) amekufa baada ya kuzikwa akiwa hai katika kaburi moja na mtu anayedaiwa kumuua kwa njia ya kishirikina.
Tukio hilo limetokea katika Kitongoji cha Maweni kijijini hapo wilayani Chunya mkoani Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani  alikiri kutokea  kwa tukio hilo akieleza kuwa lilitokea  saa 9:00 mchana katika kijiji hicho cha Maweni Mkwajuni wilayani Chunya.
“Marehemu aliuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kupigwa na mawe kwa tuhuma za kuhusika na uchawi na kusababisha kifo cha Peter Robert,” alisema.
Kamanda Athumani alisema kuwa uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea na kwamba wahusika wote wa tukio hilo wamekimbia na kuzihama nyumba zao, hivyo polisi wanaendelea na msako wa kuwatia mbaroni watuhumiwa na kwamba tayari  kaburi hilo limefukuliwa jana kutenganisha maiti hizo.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa  marehemu huyo ambaye alikuwa akituhumiwa kwa ushirikina aliwahi kuwa Katekista wa kigango hicho hadi mwaka 2007.
Wameeleza kuwa Mwamosi alikwenda kuhudhuria mazishi ya Peter  Robert (28) katika kitongoji hicho cha Maweni, baada ya kufuatwa nyumbani kwake na watu wakitaka aende kwa sababu yeye ni mmoja wa wazee wa mila katika kitongoji hicho.
“Bwana Mwamosi alikuwa akituhumiwa kwa uchawi kwa muda mrefu na wenzie wawili, hivyo alipofika makaburini ilianza minong`ono ya watu na huku wengine wakiguna na ndipo alipoombwa aingie kaburini kwa ajili ya kupokea jeneza lililobeba mwili wa marehemu Peter Robert,” alisema mkazi mmoja wa kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina moja la Joseph.
Alisema kuwa baada ya kuingia kaburini akiwa na watu wengine watatu wenzake walitoka kwa haraka na kumwacha Mwamosi peke yake ndipo kundi la watu waliokuwa eneo hilo la makaburi walianza kumshambulia kwa kumpiga mawe huku wakimwamuru akae chini.
Shuhuda huyo alisema kuwa baada ya kukubali kukaa chini akiwa ndani ya kaburi hilo, walianza kumfukia na alipofukiwa nusu ya mwili wake waliingiza jeneza la marehemu Peter na kuliweka juu yake na kuanza kulifukia kaburi hilo.
“Baada ya kukaa chini ndani ya kaburi hilo ndipo walianza kumfukia kwa udongo na baadaye wakachukua jeneza la marehemu na kuliweka juu yake, kisha kumfukia na udongo na taratibu za mazishi ziliendelea kwa ajili ya marehemu  Peter,”alisema.
Alidokeza kuwa chanzo cha tukio hilo ni marehemu Robert kuugua ghafla tumbo, ndipo ndugu zake walipoamua kumpeleka kwa mganga wa jadi kwa ajili ya kupata matibabu na baada ya siku tatu alifariki dunia.
Kamanda huyo amewasihi wakazi wa Mkoa wa Mbeya kuacha tabia kama hizo kwani kufanya hivyo ni kuuchafua mkoa na kuwa na sifa mbaya, hivyo kusababisha maendeleo ya mkoa kurudi nyuma.
Januari 12, mwaka huu wakazi wawili wa Kijiji cha Karungu, Kata ya Ivuna, Wilaya ya Momba, mkoani Mbeya walikufa baada ya kufukiwa wakiwa hai katika kaburi moja na marehemu wanaodaiwa kumuua, tukio linalohusishwa na imani za kishirikina.
CHANZO: Mwananchi
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment