![]() |
Papa Benedicto wa 16 |
Ripoti mpya inasema kuwa Papa Benedicto wa 16 aliamua kujiuzulu wadhifa wake wa kuliongoza Kanisa Katoliki baada ya kubaini kiwango kikubwa cha skendo na kashfa za masuala ya ushoga na ufisadi ndani ya Vativan.
Mnamo Februari 11, Papa Benedicto 16, ambaye ni kiongozi wa kiroho wa Wakristo, alibainisha kuwa anakusudia kujiuzulu rasmi nafasi yake itakapofika tarehe 28 Februari kwa kuwa hawezi tena kutekeleza majukumu yake kutokana na umri wake.
Hata hivyo, siku ya alhamisi ripoti hiyo iliyotolewa na gazeti la Italia la La Repubblica, ilieleza kuwa papa aliamua kujiuzulu baada ya uchunguzi wa ndani ya kanisa ulimhabarisha juu ya mlolongo wa matukio ya usaliti, mrungura na kashfa ya chini kwa chini ya ushoga ndani ya Vatican.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa makadinali watatu, akiwemo mkuu wa zamani wa masuala ya ulinzi wa Vatican, walitakiwa kuchunguza tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, ushoga na ufisadi ulioibuliwa na uchapishwaji wa nyaraka za siri za papa katika skendo ijulikanayo kama “Vatileaks.”
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, makadinali hao watatu waliwasilisha ripoti ya uchunguzi wao kwa Papa tarehe 17 Desemba, 2012 katika vitabu vikubwa viwili vyenye majalada ya rangi nyekundu, vyenye takriban kurasa 300, vilivyokuwa na "ramani halisi ya uovu na ufisadi" ndani ya Holy See.
"Ni siku hiyo, na ripoti hizo zikuwa mezani kwake, ndipo Papa Benedicto 16 alipochukua uamuzi aliokuwa ameuficha kwa muda mrefu," ilisema ripoti hiyo.
Vatileaks ilitokea Januari 2012, baada ya mlolongo wa nyaraka za ndani za Holy See zilipovuja kwenye vyombo vya habari vya Italia na kusababisha sintofahamu katika taifa zima.
Kufuatia tukio hilo, mwanahabari wa Kiitaliano, Gianluigi Nuzzi, aliongeza mafuta kwenye moto baada ya kutoa kitabu chake kiitwacho “His Holiness.”
Kitabu hicho kinaangazia vita vya madaraka ndani ya Vatican kwa kutoa nyaraka na barua za siri kutoka na kwenda kwa papa na kwa katibu wake muhtasi.
Mnamo Mei 2012, mamlaka za Vatican zilimkamata Paolo Gabriele, msaidizi wa Papa, kwa tuhuma za kuhusikana uvujishaji wa nyaraka hizo za siri akapewa adhabu ya kifungo cha miezi 18 jela. Hata hivyo, baadaye alisamehewa.
Ripoti nyingine vilevile ziliibuka katika vyombo vya habari vya Italia mwezi Juni 2012, vikiihusisha Vatican na viongozi wa kundi la mafia la Sicilia.
Ripoti hizo zilitokea baada ya kiongozi wa benki ya Vatican (Vatican Bank), Ettore Gotti Tedeschi, kufukuzwa kufuatia madai ya vita vya madaraka na ufisadi ndani ya Holy See.
Aliripotiwa kuwa chini ya uchunguzi wa tuhuma za utakatishaji wa fedha kwa ajili ya kiongozi wa kundi la Mafia.
0 comments:
Post a Comment