Walemavu wadaiwa kubakwa, kulawitiwa

VYOMBO vya dola, ikiwamo Jeshi la Polisi na Mahakama, vinachangia vitendo vya ubakaji na kulawitiwa kwa watu wenye ulemavu wa akili. Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti Taifa wa Chama Cha Walemavu wa Akili Tanzania (TAMH), Anna Mhina.

Alisema zipo kesi nyingi zinapelekwa polisi na kufikia hatua ya kusikilizwa mahakamani, lakini mara nyingi kesi hizo zinashindwa kutoa haki kwa walemavu kutokana na mifumo pamoja na urasimu.

“Kuna kesi mbili ambazo zilitokea katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke, kesi hizi walalamikaji walikuwa walemavu wa akili, walikuwa wamebakwa lakini kesi iliendeshwa na ikafika mwisho ushahidi wa wale walemavu unaambiwa hauaminiki kwa sababu wana tatizo la akili.

“Lakini kesi nyingine ilikuwa Mahakama ya Kinondoni, na yenyewe iliisha hivi hivi, lakini kitu kingine cha kusikitisha ni kwamba kuna kijana ni mlemavu wa akili huko mkoani Tabora alipata kesi kwamba amebaka na hadi leo hii amefungwa huko Tabora yuko gerezani.

“Lakini jambo la kusikitisha yule kijana kule gerezani analawitiwa kiasi kwamba hali yake ni mbaya sana, anaweza akapoteza maisha muda wowote, sasa tunajiuliza haki za hawa watu ziko wapi?

“Je, Serikali inashindwa kuweka sawa sheria ili kuwalinda watu hawa,” alihoji Mama Mhina.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Utetezi wa Haki za Wagonjwa wa Akili Tanzania (TUSPO), Eliezer Mdakilwa, alisema mifumo si rafiki katika kuwalinda watu wenye ulemavu wa akili.

Akichangia mada katika mkutano uliohusisha wadau mbalimbali wa masuala ya walemavu, Katibu wa Chama Chama Walemavu wa Uti wa Mgongo, Abdulaziz Shambe, alisema Serikali inashindwa kuwajali walemavu kwa kuweka miundombinu isiyo rafiki.

“Kama sasa hivi Serikali inazungumzia mabasi ya mwendo kasi, lakini je, wapi wameeleza kwamba mabasi haya yatakuwa na sehemu maalumu za kuwapandisha walemavu na viti vyao,” alisema Shambe.

CHANZO: MTANZANIA
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment