“Na Allah ndie mshindi kwa kila jambo lake, lakini watu waliowengi hawajui”
(Qur’an 12:21)
Kila sifa njema ni za Allah (S.W.T), muumba wa mbingu na ardhi, akaubainisha mchana kutokana na usiku akalitenganisha giza kutokamana na nuru. Sala na salamu zimuendee mbora wa walimwengu Mtume wetu Muhammad (S.A.W).
Ndugu Waislamu na Wazanzibari,
Kwa muda sasa tumekumbwa na mitihani mbali mbali katika visiwa vyetu vipenzi vya Zanzibar, mitihani hiyo ni pamoja na Kuwekwa rumande kidhulma viongozi wetu shupavu, chini ya sheria za ukafiri. Si kwa sababu nyengine ila kwa kutetea heshima ya ardhi yetu. Pia viongozi wa juu wa Serikali na vyama wameamua kuusaliti Umma wa Waislamu na Wazanziabri katika kuidai nchi yao, hili ni jambo la kusikitisha na kuhuzunisha, lakini lisituvunje moyo wala kuturudisha nyuma. Kwani kuvunjika moyo si katika tabia ya Uislamu wala Muislamu. Mtume wetu Muhammad (SAW) ametufundisha kuwa washupavu na wastahamilivu katika kuyaendea mambo yetu mema huku tukitawakkal kwa Allah muweza wa kila jambo.
Sambamba na hilo, kumekuwa na propaganda nyingi zikienezwa dhidi ya Jumuiya na Taasisi za Kiislamu na kuwa mashekhe zetu wameanza kufanyiwa wema na ihsani huko gerezani kwa kupatiwa chakula cha nyumbani. Hatuna uhakika ikiwa chakula hicho kinawafikia kikiwa salama bila ya kuingizwa kitu chenye madhara ndani yake au vinginevyo. Propaganda hizo zinalengo la kupunguza hasira na chuki za Wazanzibari zinazotokana na vitendo vinavyofanywa na SMZ, SMT na washirika wao dhidi ya Shekhe zetu, pamoja na kupunguza nguvu ya harakati za kudai nchi yetu ya Zanzibar ikiwa na mamlaka yake kamili kitaifa na kimataifa.
Jumuiya ya ya Uamasho kwa mnasaba wa yaliyojiri na kuelezwa hapo juu, inaweka bayana kwa Waislamu na Wazanzibari kwa kutamka yafuatayo:
1. Kukamatwa kwa mashekhe, viongozi au Waislamu ni dhulma na hakutaturudisha nyuma katika kudai na kutetea haki yetu ya msingi ya kuwa na Taifa letu la Zanzibar lenye mamlaka yake kamili kitaifa na kimataifa.
2. Kuruhusiwa mashekhe kupelekewa chakula kutoka nyumbani si wema wala ihsani, ni wajibu wa serikali na taasisi husika kuona viongozi wetu wanapatiwa huduma zote muhimu bali pia iwaachie huru bila ya masharti kwa vile imewashikilia chini ya mfumo wa dhulma na ukafiri.
3. Waislamu hawatarudi nyuma kwa kufungwa viongozi wao au venginevyo, ila wataendelea kudai haki kwa nguvu zao zote kwa mtu mmoja mmoja au kikundi, hadi nchi yetu ya Zanzibar ipatikane huku tukiendelea kuomba msaada wa Allah (SWT) katika kurahisisha kupatikana kwa nchi yetu kipenzi.
4. Waislamu waelewe ya kwamba hakuna mfumo wowote unaoweza kusimamia haki na kuikomboa nchi yetu ya Zanzibar ikiwa ni mfumo wa kijamaa, wa kidemokrasia au mfumo mwengineo kinyume na Uislamu ulio sahihi. Hivyo tushikamane na Uislamu katika kuidai nchi yetu kwa hali na mali.
5. Nusra ya nafsi na nchi yetu inatoka kwa Allah (‘Azza wajalla), tuhakikishe Allah pekee ndio ngao yetu dhidi ya dhulma tunazofanyiwa Waislamu na Wazanzibari kwa ujumla.
Wabillah Taufiq
“Ewe Allah tunakuomba utuunganishe na utuimarishe katika msimamo wetu huu wa kudai haki yetu na uwabainishe, uwaumbue na uwadhalilishe madhalimu wote na vibaraka wao kama wanavyowadhalilisha Uislamu, Sekhe zetu na Zanzibari kwa ujumla.” Amin Amin Amin.
Uamsho Media Center 14/ Saffar/ 1434
About mahamoud
This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:
Post a Comment