*Yataka iitwe Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
*Yasisitiza isiingiliwe na mamlaka yoyote nchini
* Lubuva: Wajumbe wa tume waapishwe na Jaji Mkuu
*Apendekeza mbunge asivuliwe ubunge akihama chama
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imependekeza kuitwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambayo haitaingiliwa na mamlaka yoyote nchini katika utekelezaji wa majukumu yake.
Pia, imependekeza wake waapishwe na Jaji Mkuu badala ya Rais ili kuondoa dhana kwamba wajumbe wa tume watakuwa na utii kwa Rais ambaye ni mwenyekiti wa chama tawala.
Akiwasilisha maoni ya NEC kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema pamoja na mambo mengine tume pia imependekeza uwepo utaratibu maalum utakaowawezesha wajumbe wa tume huru kuthibitishwa na Bunge kabla ya kuteuliwa na Rais.
“Tume inapendekeza mchakato wa uteuzi wa wajumbe wake kuanzia kwenye kamati itakayojumuisha wataalam wa mambo ya uchaguzi, sheria, siasa na jamii kwa ujumla na mapendekezo hayo yapelekwe kwenye jopo maalum litakalojumuisha Watanzania wanaokubalika na jamii na kisha kupelekwa bungeni kabla ya kuwasilishwa kwa Rais kwa ajili ya uteuzi rasmi.
“Vyombo hivi vitatu kwa pamoja katika hatua tatu tofauti vitakuwa na jukumu la kupendekeza majina ya wajumbe wa tume huru ambao majina yao yatawasilishwa kwa Rais aweze kumteua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti miongoni mwao.
“Kuhusu suala la Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa tume kutoka upande mmoja wa Muungano, tume inashauri uendelee kutumika utaratibu unaoelezwa katika katiba ya sasa.
“Tume imependekeza kuwa sifa za wajumbe zisijielekeze kwenye elimu peke yake bali hata sifa nyingine za uadilifu, heshima, uwajibikaji na kukubalika kwa mtu katika jamii ziwe ni miongoni mwa sifa kwa mtu kuomba na kuteuliwa kuwa mjumbe wa tume na muda wa kukaa madarakani baada ya kuteuliwa uendelee kuwa miaka mitano,” alisema Jaji Lubuva.
Alisema tume pia imependekeza Mbunge kutonyang’anywa nafasi yake ya uwakilishi endapo atahamia chama kingine au kufukuzwa na chama chake.
Hatua hiyo itasaidia kupunguza wingi wa uchaguzi mdogo usio wa lazima badala yake uchaguzi mdogo ufanyike mwakilishi atakapofariki dunia au kuondolewa na Mahakama.
“Ingawa tume inapendekeza kuendelea kwa utaratibu wa uchaguzi mdogo bado kuna umuhimu wa katiba mpya kutoa utaratibu kwa kudhibiti vyama vya siasa na wanasiasa kuhama au kufukuzana ndani ya vyama bila kuathiri nafasi ya uwakilishi ya kiongozi husika,” alisema.
Kuhusu uchaguzi, tume ilipendekeza katiba mpya kuipa tume mamlaka ya kusimamia uchaguzi wote hadi wa Serikali za Mitaa tofauti na sasa ambako inasimamia uchaguzi mkuu pekee kuanzia ngazi za madiwani.
Kwa upande wa viti maalum vya wanawake, tume ilipendekeza ipewe mamlaka ya kuandaa utaratibu maalum wa kuwapata wagombea wa nafasi hizo katika vyama vyote vya siasa kuondoa malalamiko juu ya mfumo wa uliopo sasa ndani ya vyama vya siasa.
Pia NEC imependekeza ianzishwe mahakama ya mambo ya uchaguzi ambayo itawezesha watu kuwasilisha malalamiko yao kabla ya uchaguzi.
Mahakama hiyo itakuwa na kazi ya kuendesha kesi dhidi ya ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi wakati na baada ya uchaguzi, kusikiliza kesi za uchaguzi kwa haraka na muda mfupi tofauti na sasa ambako inaendeshwa mwaka mmoja au miwili huku Jimbo au Kata likibaki bila mwakilishi.
“Katika ukomo wa muda wa kugombea nafasi za Ubunge/Udiwani, tume inaona kuwa si vema kuweka ukomo wa muda kwa watu kushika nafasi hizo ukizingatia umri wa kugombea ni miaka 21. Iwapo mtu atashika nafasi husika akiwa na miaka 21 na akiwa katika nafasi hiyo kwa vipindi viwili ina maana atamaliza akiwa na miaka 31, sasa kumzuia mtu huyu asigombee tena itakuwa ni kumnyima haki yake bila sababu za msingi.
“Tume inakiri kwamba baadhi ya majukumu ya tume na Msajili wa Vyama zimekuwa zikishabihiana ingawa kuna tofauti kati yake kwa sababu tume inahusika na uchaguzi na Msajili anahusika na vyama tu, ieleweke wazi kwamba haijawahi kutokea mgongano katika utekelezaji wa ofisi hizi mbili.
“Hivyo tume inapendekeza ofisi hizi zibaki kuwa kama ilivyo sasa kutokana na ukweli kwamba majukumu ya ofisi ya Msajili yameongezeka baada ya kuanzishwa kwa sheria ya gharama za uchaguzi ambazo Msajili ana jukumu la kusimamia.
“Kutokana na umuhimu wa elimu ya uraia kwa wananchi, katiba mpya itoe mwongozo na ianzishe chombo kitakachohusika rasmi na utoaji wa elimu ya uraia itakayosimamiwa na tume kama ilivyo kwa nchi za Afrika Kusini, Madagascar, Malawi, Botswana, Angola na Zambia,” alisema Jaji Lubuva.
CHANZO: MTANZANIA
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment