![]() |
| Wapalestina wakisherehekea kuanza kwa makubaliano ya amani na Israeli mjini Gaza Jana. |
Mamia ya Wapalestina walimiminika katika mitaa ya Gaza na Ukanda wa Magharibi kusherehekea makubaliano ya amani yaliyohitimisha hujuma za kijeshi dhidi ya ukanda huo uliozingirwa.
Wakiimba nyimbo za ushindi na nara za "muqawama umeshinda," wakazi hao waliokuwa na furaha walifurika katika mitaa ya Ukanda wa Gaza usiku wa kuamkia leo kuonesha furaha yao juu ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa Misri, ambayo yalianza kutekelezwa saa 3:00 usiku kwa majira ya eneo hilo.
"Tulikuwa kifungoni. Nimefurahishwa mno na kuhitimishwa kwa mabomu na vita," alisema Nasim Hamduna, mkazi wa Ukanda wa Gaza.
"Niliyaacha makazi yangu wakati wa vurugu na sasa ninareje," aliongezea kusema kwa furaha.
Ahmed Bahr, afisa mwandamizi wa Hamas, alipongeza makubaliano hayo, akisema: "Makundi ya muqawama yamefanikisha ushindi wa kihistoria na kuandaa njia ya mapambano ya kuikomboa Palestina."
Furaha kama hiyo ilionekana pia katika miji mingine Ukanda wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Mapema Jumatano, Misri ilitangaza kuwa utawala wa Israeli na wapambanaji wa Kipalestina wa Hamas walifikia makubaliano ya kusitisha mapambano.
Chini ya mapatano hayo, Wapalestina na Waisraeli wamekubaliana kusitisha uhasama wote baina yao. Vilevile Israeli imekubali kufungua njia zote na kurahisisha harakati za watu na mizigo ndani na nje ya Ukanda wa Gaza. Lakini haikukubali kuondosha mzingiro iliyouweka kwa Ukanda huo.
Hujuma za mashambulizi mazito ya utawala wa Israeli yaliwaua zaidi ya Wapalestina 160 na kuwajeruhi wengine wapatao 1,200 tangu Novemba 14.


0 comments:
Post a Comment