 |
Dkt. Shukuru J. Kawambwa (Mb) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi |
Shule ya Sekondari Bagamoyo ni shule ya bweni, ya mchanganyiko, yaani yenye wasichana na wavulana. Shule hii ina wanafunzi wa kidato cha Tano na Sita pekee. Jumla ya wanafunzi wote ni 760 na kati yao 100 ni wasichana na wavulana ni 660. Shule hii ina jumla ya walimu 65 ambapo walimu wa kike ni 36 na wa kiume ni 29. Tarehe 5/11/2012 Shule hiyo ilifungwa kutokana na kuwepo kwa dalili za kuvunjika kwa amani na utulivu shuleni hapo. Baada ya shule kufungwa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliunda Kamati ili kuchunguza nini hasa chanzo cha mgogoro uliopelekea hata kuwepo kwa dalili za kuvunjika amani na utulivu shuleni hapo. Kamati imekamilisha kazi yake ikiwa na taarifa nzima ya mwenendo wote wa mgomo na vurugu zilizotokea. Katika uchunguzi imebainika kuwa chanzo kikuu cha vurugu hizo ni mfarakano kati ya uongozi wa shule na baadhi ya wanafunzi. Mfarakano huo ulitokana na wanafunzi kutokubaliana na mabadiliko ya kinidhamu ambayo Mkuu wa Shule aliyaanzisha. Aidha, Kamati imegundua kuwa kukosekana kwa umoja wa kikazi miongoni mwa walimu, utoro wa walimu kazini na utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wanafunzi kumechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa mgogoro huo. Baada ya kupitia kwa makini hali halisi ya mgogoro huu, Serikali imeamua yafuatayo: 1. Ili kutoa nafasi kwa uongozi wa shule kujipanga upya, wanafunzi wote waliothibitika kutoshiriki katika mgomo watarudi shuleni mapema mwezi Januari 2013 kwa utaratibu watakaotangaziwa. 2. Wanafunzi wote waliothibitika kuwa vinara wa vurugu watachukuliwa hatua za kinidhamu. 3. Walimu walioonekana kutokuwajibika ipasavyo watachukuliwa hatua stahiki za kinidhamu. Aidha, Serikali inaagiza kwamba Wakuu wote wa Shule wachukue hatua za haraka na watoe taarifa kwa viongozi wa Halmashauri za Wilaya na Mikoa pindi wanapogundua dalili za mgogoro ili hatua stahiki zichukuliwe mapema. Vile vile wanafunzi wote wanakumbushwa na kuagizwa kwamba kushiriki katika migomo ni kuvunja sheria za shule na wanapoteza muda wa masomo yao. Watumie njia halali kufuatilia mahitaji yao.
Dkt. Shukuru J. Kawambwa (Mb)
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi
24/11/2012
This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
0 comments:
Post a Comment