![]() |
| Madaktari wa Kipalestina wakiwa wamempeleka mtoto aliyejeruhiwa katika Hospitali ya al-shifa hospital Mjini Gaza kufuatia mashambulizi ya anga yaliyofanywa na ndege za Israeli Novemba 14, 2012. |
NA KABUGA KANYEGERI
MISRI imemrejesha nyumbani balozi wake wa Israeli katika kupinga mashambulizi mapya ya anga yaliyofanywa na Tel Aviv kwenye Ukanda wa Gaza.
Jana Jumatano, Rais wa Misri, Mohamed Morsi aliagiza "kurejeshwa nyumbani balozi wa Misri nchini Israeli," msemaji wa rais, Yasser Ali alisema hayo katika taarifa iliyotangazwa na televisheni ya serikali.
"Rais Mohamed Morsi amefuatilia mashambulizi ya kinyama ya Israeli yaliyoua idadi kadhaa ya mashahidi na watoto wa Kipalestina," Ali aliongeza kusema.
"Kwa msingi huu amemrejesha nyumbani balozi wa Misri kutoka Israeili; amemuagiza mwakilishi wa Misri kwenye Umoja wa Mataifa kuitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama," ilisema taarifa hiyo.
Vile vile Morsi aliiagiza wizara ya Mambo ya Nje kumuita balozi wa Israeli nchini Misri kumhoji juu ya mashambulizi hayo na akataka kufanyika kwa kikao cha dharura cha mawaziri wa Jumuiya ya Umoja wa nchi za Kiarabu mjini Cairo kujadili mashambulizi hayo ya Israel.
Balozi wa Israeli nchini Misri, Yaakov Amitai aliondoka Misri baada ya Rais Morsi kutangaza kuwa alikuwa akimuita.
"Kwa niaba ya wananchi wa Misri, Rais anatoa rambirambi kwa wananchi wa Palestina kwa maujai ya mashahidi wao," alisema Ali.
Mapema siku hiyo hiyo, Wamisri walifanya maandamano ya kuipinga Israeli katika Meidani ya Tahrir mjini Cairo, wakiitaka nchi yao imrejeshe nyumbani balozi wao kutoka Tel Aviv kufuatia mashambulizi ya kinyama ya ndege za Israeili.
Jana Jumatano, Israeli ilianzisha operesheni kubwa ya kijeshi dhidi ya Ukanda wa Gaza na kuwaua watu kumi akiwemo Kamanda mwandamizi wa Hamas, Ahmed al-Ja'bari.
Wapalestina kumi pia walijeruhiwa katika mashambulizi hayo. Watoto wawili ni miongoni mwa waliouawa katika mashambuli hayo, kwa mujibu wa waziri wa afya wa Gaza.
Tel Aviv imeendelea kushambulia kutoka angani na baharini na imeenda mbali zaidi kwa kuyaita majeshi yake ya akiba ili kufanya uvamizi wa ardhini.
Mara kwa mara jeshi la Israeli limekuwa likifanya mashambulizi ya anga na mengine dhidi ya Gaza kwa madai kuwa mashambulizi hayo yanafanywa kwa malengo ya kujilinda. Lakini nguvu kubwa imekuwa ikitumika na kuvunja sheria ya kimataifa na raia wengi wamekuwa wakiuawa au kujeruhiwa.
Gaza imekuwa katika mzingiro tangu mwaka 2007, hali iliyosababisha kuporomoka kwa kiwango cha maisha, ongezeko la ukosefu wa ajira na umaskini.

0 comments:
Post a Comment