Aliyewahi kuwa Rais wa Iran Hashemi Rafsanjani amefariki
dunia akiwa na umri wa miaka 82 kutokana na mshituko wa moyo.
Rafsanjani alipelekwa hospitali moja kaskazini mwa mji
wa Tehran baada ya kusumbuliwa na tatizo hilo.
Mwanasiasa huyo mashuhuri aliyezaliwa Agosti 25, 1934, alikuwa
rais wa nne wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyehudumu kuanzia mwaka 1989 mpaka
1997.
Rafsanjani alikuwa mkuu wa Baraza la Wataalamu kuanzia
mwaka 2007 mpaka 2011. Mwanadini huyo alichaguliwa kuwa spika wa bunge la Iran
mwaka 1980 nafasi aliyoendelea kuishikilia mpaka mwaka 1989. Aliteuliwa kuwa
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kuanisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu nchini humo
mwaka 1989.
Ayatollah Hashemi Rafsanjani alikuwa miongoni mwa
wasaidizi waandamizi wa kiongozi wa zamani wa taifa hilo, Hayati Imam Khomeini.
Alikuwa na mchango mkubwa wakati wa mapambano ya kupinga
utawala wa mfalme Shah kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na baadaye
katika hatua mbalimbali za kuasisiwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Wakati wa vita vya Iraq na Iran vilivyodumu kwa muda wa
miaka 8, Rafsanjani alichukua nafasi ya kaimu amiri jeshi mkuu wa vikosi vya
majeshi ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran (IRNA), mazishi
ya Hashemi Rafsanjani yatafanyika siku ya Jumanne mjini Tehran.
0 comments:
Post a Comment