Mahakama nchini Uganda imetoa kibali cha kukamatwa kwa
mwanamuziki maarufu wa Nigeria, Wizkid, kwa kushindwa kutoa kwenye onesho la
burudani.
Kibalo hicho kinamtaka afisa yeyote wa polisi kutoka
Uganda au polisi ya Kimataifa (Interpol) kumkamata Wizkid na kumfikisha
mahakamani kabla ya tarehe 16 Januari mwaka 2017.
Waganda walisikitishwa na kitendo cha mwanamuziki huyo
kutooneka kwenye onesho la muziki lililopangwa kufanyika tarehe 3 Desemba
katika Uwanja wa Cricket wa Lugogo mjini Kampala.
Kibali hicho kimetolewa kwa msingi kwamba muimbaji huyo
alijipatia pesa kwa njia ya hila, udanganyifu na kufanya hujuma. Mbali na
mashitaka hayo, waandaaji wa tamasha hilo, Face TV na wanasheria wanataka
ahukumiwe kifungo cha miaka 11 jela iwapo hatarejesha fedha alizolipwa.
Licha ya kuwasababishia hasara ya tiketi za kiingilio na
tiketi ya ndege, gharama za hoteli, eneo na matangazo ambayo yaligharimu zaidi
ya dola 300,000, waandaaji wa onesho hilo pia walimlipa meneja wa Wizkid dola 60,000
kama malipo yake ya kutumbuiza, dola 5000 ya udalali na dola 3000 za matumizi kwa
siku zote ambazo mwanamuzi huyo na timu yake wangekaa nchini humo. Aidha, zaidi
ya watu 25,000 walikuwa wamenunua tiketi ili kushuhudia onesho hilo.
Kwa mujibu wa mtandao wa Mediamax, hivi karibuni Wizkid alikuwa
nchini Marekani kwa sababu za kimatibabu na kwa mujibu wa waandaaji, Wizkid hakuweza
kupanda ndege kutoka Marekani mpaka Uganda kutokana na “mazingira yasiyoepukika”.
0 comments:
Post a Comment