Etienne Tshisekedi, kiongozi wa chama cha upinzani cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo |
Chama kikuu cha upinzani katika nchi ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo kimewataka wananchi kutomtambua Joseph Kabila kama rais, kikiwataka
kufanya maaandamano ya amani kumpinga.
Kiongozi wa chama cha Union for Democracy and Social
Progress (UDPS), Etienne Tshisekedi, amekiita kitendo cha Kabila kubaki
madarakani kuwa ni kinyume na sheria na ni kitendo haramu na kwamba ni sawa na
mapinduzi ya kijeshi.
Rais Kabila aliingia madarakani mwaka in 2001, mara
baada ya kuuawa kwa baba yake. Mwaka 2006, mabadiliko ya katiba yalifanyika na
kuweka ukomo wa urais kuwa vipindi viwili tu ambapo leo tarehe 20 ndio siku ya
mwisho kikatiba ya kuhudumu kama rais na hivyo kumzuia kugombea kwa muhula wa
tatu lakini amegoma kuachia ngazi.
Mnamo mwezi Oktoba, tume ya uchaguzi nchini humo ambayo
inalaumiwa na vyama vya upinzani kuwa inashirikiana na Kabila, ilitangaza
kuahirisha uchaguzi ambao ungefanyika Desemba 2016 na kuusogeza mbele mpaka
Aprili 2018, na hivyo kumpa fursa bwana Kabila mwenye umri wa miaka 45
kuendelea kubaki madarakani.
Uamuzi wa tume hiyo na ule wa bwana Kabila wa kuendelea
kubaki madarakani uliwakasirisha wapinzani, hasa katika mji mkuu Kinshasa, na
hivyo kuitumbukiza nchi hiyo katika mzozo wa kisiasa na kuibua ghasia za mara
kwa mara kwa kipindi cha miezi miwili sasa.
Mnamo mwezi Septemba yaliibuka makabiliano kati ya
polisi na waandamanaji mjini Kinshasa waliokuwa wakimtaka Kabila kujiuzulu. Zaidi
ya watu 50 walipoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Leo Tshisekedi mwenye umri wa miaka 84 aliitolea wito
Jumuiya ya Kimataifa kutoendelea kushirikiana na Joseph Kabila kama Rais wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Taarifa zinasema kuwa japokuwa serikali imepiga marufuku
maandamano, waandamanaji wamekuwa wakifanya maandamano nchi nzima kwa siku
kadhaa sasa na waandamanaji kadhaa wametiwa nguvuni hasa katika mji wa Goma
mashariki mwa nchi hiyo.
Japokuwa Tshisekedi amewataka watu kuandamana kwa amani
dhidi ya bwana Kabila, ujumbe wake wa video unaweza kuitumbukiza nchi hiyo
katika ghasia zaidi kwa sababu Rais amedhamiria kukabiliana na upinzani wowote
dhidi ya mamlaka yake.
Nchi hiyo iliwahi kukumbwa na matatizo mengi kwa miongo
kadhaa hususan vita katika eneo la mashariki ambavyo vililipuka tangu mwaka 1998
na kusababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 5.5.
Makumi ya makundi ya waasi yamekuwa yakiendesha harakati
zake katika eneo la mashariki tangu wakati huo, na jeshi la serikali likiungwa
na vikosi vya Umoja wa Mataifa limekuwa likipambana na waasi hao.
Waasi hao wamekuwa wakituhumiwa kufanya mashambuli na
vitendo vya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na ubakaji na
kuwasajili watoto katika jeshi.
0 comments:
Post a Comment