Picha kutoka televisheni ya serikali iliyopigwa Desemba 2, 2016 ikimuonesha Rais wa Gambia Yahya Jammeh akizungumza baada ya kushindwa katika uchaguzi wa urais. |
Rais wa Gambia Yahya Jammeh ameyakataa matokeo ya
uchaguzi wa urais uliofanyika hivi karibuni nchini humo wiki moja baada ya
kukubali kushindwa na mpinzani wake.
"Hivyo basi ninatangaza kuyakataa matokeo yote,"
Jammeh alisema katika taarifa iliyorushwa kwenye kituo cha televisheni cha
serikali usiku wa kuamkia leo, akisisitiza kuwa uchunguzi uliofanywa tangu
Desemba mosi umeonesha kuwa kulikowa na ukiukaji wa taratibu katika uchaguzi
huo, jambo ambalo amesema kuwa halikubaliki.
"Ninarudia: Sitayakubali matokeo kutokana na
kilichotokea," aliongeza Jammeh ambaye ameitawala nchini hiyo ya Afrika
Magharibi kwa zaidi ya miaka 22.
Wakati wa taarifahiyo, kiongozi huyo alieleza kuwa
baadhi ya taarifa katika matokeo ya uchaguzi zilifanyiwa hila na kwamba wapiga
kura walinyimwa haki ya kupiga kura.
"Uchunguzi wetu umebaini kuwa katika baadhi ya
matukio wapiga kura waliambiwa kwamba tayari upinzani ulikuwa umeshinda na
hivyo hawana haja ya kupiga kura, hivyo baadhi yao kwa hasira wakarudi nyumbani,"
Jammeh alisema.
Wafuasi wa upinzani wakishangilia baada ya kiongozi wao Ousainou Darboe pamoja na wapinzani wengine 18 kuachiwa huru kwa dhamana mnamo Desemba 5, 2016 mjini Banjul, siku chache tu baada ya upinzani kushinda uchaguzi. |
Kauli hiyo inakuja ikiwa imepita wiki moja tu tangu
alipoonekana katika televisheni ya serikali akimpigia mgombea wa upinzani Adama
Barrow na kumtakia kila la heri huku akionekana kuwa mwenye furaha.
"Wewe ni rais mteule wa Gambia, nami ninakutakia kila
la heri," Jammeh alimwambia Barrow siku hiyo na kuongeza kuwa hana
kinyongo naye.
Uamuzi huo wa kurudi nyuma unatarajiwa kuibua ghadhabu
na hasira miongoni mwa wapinzani na idadi kubwa ya Wagambia wanaoishi
uhamishoni katika mataifa ya nje.
Hayo yanatokea wakati ambapo wiki moja tu baada ya Jammeh
kukubali kushindwa, makumi ya wafungwa wa kisiasa wameachiwa huru kwa dhamana.
Kinachosubiriwa ni kuona iwapo taifa hilo la Afrika
Magharibi lenye raia milioni 1.9 litavumilia kumuona Jammeh akiendelea
kutawala.
Kufuatia matokeo ya uchaguzi wa wiki iliyopita, Wagambia
walimiminika barabarani wakiimba na kucheza huku wakipiga nara za “Uhuru!”
Serikali za mataifa ya magharibi zimekuwa zikiukosoa
vikali utawala wa Jammeh, hasa uamuzi wake wa kujiondoa kwenye umoja wa Jumuiya
ya Madola ambao unazihusisha nchi zilizowahi kutawaliwa na Uingereza na uamuzi
wake wa kujiondoa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Wakati akitangaza nchi yake kujiondoa katika Jumuiya ya
Madola mwaka 2013, Jammeh aliielezea jumuiya hiyo kama “taasisi ya ukoloni
mambo leo.” Pia mwezi Oktoba alitangaza kuwa Gambia itajiondoa ICC akiituhumu
kuwa ni “Mahakama ya Kimataifa ya Ubaguzi.”
0 comments:
Post a Comment