WENGI WAZIDI KUFA KWA EBOLA, HALI YAZIDI KUWA MBAYA

Athari ya Ugonjwa wa Ebola


Idadi ya vifo kutokana na ugonjwa wa Ebola ulioikumba Sierra Leone imeongezeka mara dufu huku mashirika ya kimataifa yakipambana kukabiliana na virusi vya ugonjwa huo vinavyosambaa katika eneo la Afrika Magharibi.

Wizara ya Afya nchini humo imesema kuwa watu wengine sita wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo hatari baada ya wale waliofariki wiki jana.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa taasisi ya kuzuia na kudhibiti Ebola nchini humo, Amara Jambai, kwa sasa kuna kadhia 133 za ugonjwa huo ambapo kadhia 42 zimeshathibitishwa.

Hayo yanatokea wakati ripoti mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO), iliyotolewa Juni 4, ikisema kuwa kwa uchache watu 208 wamepoteza maisha katika nchi jirani ya Guinea kutokana na Ebola.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linasema kuwa kuna kadhia 328 za ugonjwa huo zilizothibitishwa au kushukiwa, ikiwa ni pamoja na vifo 208, katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Aidha, virusi hivyo vimeshagharimu maisha ya watu tisa katika nchi nyingine ya Liberia.

Kwa sasa hakuna tiba maalumu ya ugonjwa wa Ebola, ambao dalili zake ni pamoja na kuhara, kutapika na kuvuja damu.

Virusi hivyo huambukiza kwa kugusana moja kwa moja na damu iliyoambukizwa, kinyesi au jasho lake. Vilevile vinaweza kuambukiza kwa uhusiano wa kijinsia au kuzigusa maiti za waathirika bila kizuizi.

Kwa mara ya kwanza Ebola iligunduliwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwaka 1976 ambapo iliwaua watu 280.


Ugonjwa huo umeendelea kuwa miongoni mwa magonjwa hatari zaidi duniani ambapo huua kati ya asilimia 25 mpaka 90 ya wale wanaougua.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment