Moto mkubwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Jinnah mjini Karachi Pakistan baada ya wanamgambo wa Kitaliban kuushambulia usiku wa kuamkia leo. |
Usiku wa
kuamkia leo wanamgambo waliuvamia uwanja wa ndege mkubwa zaidi nchini Pakistan
na watu wasiopungua 26 wameripotiwa kuuawa katika mapigano ya usiku kucha.
Shambulizi hilo
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jinnah mjini Karachi, mji ambao ni
kitovu cha uchumi wa Pakistan wenye wakazi milioni 18, limetokea huku serikali
ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Nawaz Sharif ikijaribu kufanya mazungumzo na
wapiganaji wa Taliban kwa lengo la kukomesha mapigano yaliyodumu kwa miaka
mingi.
Shambulizi hilo
lilianza majira ya saa 5 usiku kwa majira ya Afrika Mashariki baada ya
wanamgambo 10 waliovaa sare za jeshi walipoingia kupitia lango la zamani la
uwanja huo linalotumiwa na watu maalumu.
Kundi la
Taliban nchini Pakistan, ambalo ni muungano wa makundi yanayopigana kuiangusha
serikali ya Pakistan, limeripotiwa kudai kuhusika na shambulizi hilo kwa kile
ilichokieleza kuwa ni ulipizaji kisasi dhidi ya mashambulizi yanayofanywa na
jeshi la serikali dhidi ya ngome zao kwenye mpaka wa nchi hiyo na Afghanistan.
“Huu ni ujumbe
wa serikali ya Pakistan kuwa bado tuko hai na ni jibu dhidi ya mauaji ya watu
wasiokuwa na hatia katika mashambulizi ya mabomu yanayofanywa na serikali
kwenye vijiji vyao,” alisema Shahidullah Shahid, msemaji wa kundi la Taliban.
Shambulizi hilo
linaonekana kuwa pigo kubwa dhidi ya serikali ya Sharif ambaye aliingia
madarakani kwa ahadi ya kufanya mazungumzo ya amani ili kupata suluhu ya ghasia
za miaka mingi nchini humo.
Katika uwanja
wa ndege mapigano yaliendelea kwa muda wa saa tano na picha za televisheni
zilionesha moto mkubwa huku magari ya wagonjwa yakifanya kazi ya kuondoa
majeruhi. Kwa uchache milipuko mitatu mikubwa ilisikika wakati wanamgambo
waliovaa mabomu walipojilipua.
Leo asubuhi
jeshi lilidai kuwa uwanja huo ulikuwa salama lakini moshi mkubwa ulionekana
ukifuka juu ya jengo la uwanja huo.
Msemaji wa
jeshi amenukuliwa akisema kuwa wanamgambo kumi wenye umri kati ya 20 na 25
wameuawa na vikosi vya jeshi huku kiasi kikubwa cha silaha na risasi kikipatikana
kutoka kwa wapiganaji hao.
Taarifa ya
jeshi inasema kuwa washambuliaji hao wana asili ya nchi ya Uzbekistan. Maafisa wa
Pakistan wamekuwa wakiwalaumu wapiganaji wa kigeni wanaopewa mafunzo katika
eneo la mpaka wa nchi hiyo na Afghanistan ambao wanadaiwa kupambana upande wa
Taliban.
Wakati wa
shambulizi hilo safari zote za ndege katika uwanja huo zilikuwa zimezuiwa na
hakuna taarifa za ndege yoyote kuharibiwa.
Mazungumzo ya
amani kati ya serikali na wapiganaji wa Taliban nchini humo yameshindwa katika
miezi ya hivi karibuni na hivyo kuua matumaini ya kupatikana suluhu ya uasi
unaoikabili nchi hiyo kwa muda mrefu.
Taliban wa Pakistan
ni washirika wa Taliban wa Afghanistan.
0 comments:
Post a Comment