Wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ndani na nje ya
Bunge hilo, wakiongozwa na vigogo wake, jana walifunika Zanzibar, huku kila
mmoja akisisitiza msimamo wa umoja huo wa kupinga ule wa wenzao wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wa mfumo wa Muungano wa serikali mbili.
Vigogo wa Ukawa, wakiongozwa na Freeman Mbowe, Profesa
Ibrahim Lipumba, James Mbatia, Tundu Lissu na Ismail Jussa Ladhu, na kuungwa
mkono Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad na
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, Hassan Nassoro Moyo, walisisitiza msimamo
wa umoja huo wa kutaka kuwapo mabadiliko ya kuwapo mfumo wa Muungano wa
serikali tatu.
Msimamo huo ulisisitizwa jana katika mkutano wa hadhara,
ambao ni wa kwanza wa umoja huo kufanyika tangu wafuasi wake waamue kujitoa
katika Bunge hilo, uliohudhuriwa na maelfu ya watu mjini Unguja na vitongoji
vyake, katika uwanja wa Demokrasia Kibandamaiti.
HASSAN NASSORO MOYO
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, Hassan Nassoro Moyo,
alisema serikali tatu ndiyo msimamo wa Wazanzibari na kwamba, hawawezi kubadilika.
Alisema walichagua kuungana na Watanganyika kwa sababu
ya maisha ya Wazanzibari.
MAALIM SEIF
Katibu Mkuu wa Cham cha Wananchi (CUF), Maalim Seif
Sharif Hamad, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar (SMZ), alisema serikali tatu hazina mjadala.
Hivyo, akasema kwa kuwa wenzao (CCM) wamekuwa
waking’ang’ania mfumo wa Muungano wa serikali mbili, anaukubali, lakini kwa
sharti kwamba, Zanzibar inakuwa huru.
Maalim Seif alisema kama gharama ndizo zinazoogopwa,
basi kila mtu awe na serikali yake.
Aliwashukuru viongozi wa Ukawa kwa kuonyesha uongozi
katia Bunge hilo na kusema wanaojiita wengi wameonekana wengi hivyo na
wanaonekana wachache wameonekana wachache makini.
Alisema Wazanzibari wanawaunga mkono mia kwa mia na kwa
uamuzi waliyoyachukua ya kuondoka bungeni, kwa kuwa ni uamuzi wa kijasiri na
hekima.
Maalim Seif alisema anajua zitafanywa juhudi zote
kuvunja umoja wao, kwa kutumia fedha na vitisho, lakini akawataka waendelee
kuulinda umoja wao kama mboni ya jicho.
Aliwataka kuulinda umoja wao na kuwa makini kwa kuwa hao
hawana hoja kwa kuwa mfumo wanaoutetea ni wa dhuluma na wao wanatetea mfumo wa
haki na kwamba, watashinda na hilo hana wasiwasi nalo hata kidogo.
Alisema anashangazwa kutajwa katika Bunge hilo wakati
yeye siyo mbunge.
“Msikubali na tusikubali kugawiwa,” alisema Maalim Seif.
Alisema msimamo wake ni ule wa Ukawa na kwamba, yeye
hana historia ya kuwasaliti wananchi na hayuko tayari kwa hilo.
Maalim Seif alisema Muungano uliopo ni wa nchi mbili na
kwamba, kauli ya baadhi ya viongozi wa serikali kwamba, hawawezi kuiacha
Zanzibar na kuhoji “Je, Zanzibar ni koloni lenu?”
Alitoa mfano wa Algeria, ambako wakoloni Wafaransa
waligoma kuiachia huru nchi hiyo, lakini mwisho wake waliondoka na kuiacha.
Alisema wakati wa kutishana umekwisha na kwamba vitisho
vyao haviwezi kuwarudisha nyuma Wazanzbari.
“Serikali mbili mnazozitaka nyinyi, tunasema
no,”alisema.
Kuhusu vitisho vya kumdhibiti yeye (Maalim Seif),
alisema kamwe hilo hawaliwezi.
Alisema anayo taarifa kwamba, askari wa Kikosi Maalumu
cha Kuzuia Magendo (KMKM) na Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) wamekuja katika
eneo la mkutano wakiwa wamevalia kiraia ili wawasumbue wananchi barabarani
baada ya mkutano.
Alisema yeye kama Makamu wa Kwanza wa Rais, anaamuru
askari hao waondolewe mara moja eneo hilo, vinginevyo watamjua Maalim Seif kuwa
ni nani?
JAMES MBATIA
James Mbatia
ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na Mbunge wa Kuteuliwa na Rais aliwaonya
wawakilishi wa Ukawa Zanzibar juu ya kitendo cha kuiuza Zanzibar ili kujenga
uhusiano mwema kati yao na wenzao wa Tanganyika.
“Tusikubali katu katu hatua tuliyofikia kurudi nyuma,
Mwenyezi Mungu atatoa baraka zote na kugombana naye, ” alisema Mbatia.
FREEMAN MBOWE
Freeman Mbowe, ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema na Mbunge
wa Hai, alisema kauli kwamba, Ukawa wakirudi kwa wananchi watachekwa ni dalili
kwamba, utawala umekosa busara.
Alisema leo wataendelea na mikutano kisiwani Pemba na
baada ya hapo watakwenda jijini Dar es Salaam kuhakikisha haki ya wananchi
inapatikana.
Mbowe alisema Zanzibar ndiyo itakayoonyesha njia ya
kufanikisha harakati za kufikia lengo la kuwapo kwa mfumo wa serikali tatu.
Alisema wako tayari kuendelea kutukanwa, lakini
watatembea nchi nzima kuhakikisha wanadai haki za Watanzania, ikiwamo serikali
tatu.
KUVUNJA BARAZA LA MAWAZIRI
Alisema ushirika uliopo baina vyama vyao hivi sasa,
hautaishia tu katika kudai katiba ya wananchi, bali utaendelea hadi katika
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia na katika Uchaguzi Mkuu ujao wa
mwaka 2015.
Mbowe alisema kwa kuzingatia hilo, wiki ijayo atavunja
baraza la mawaziri kivuli linaloundwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na
kuliunda upya ili kuhakikisha Ukawa inasambaa siyo katika Bunge Maalumu la
Katiba tu, bali unaendelea pia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na katika Uchaguzi Mkuu mwakani.
“Nina imani mwaka 2015 tunaendelea kuzungumza,
tutakwenda kwenye uchaguzi tukiwa kitu kimoja,” alisema Mbowe.
PROFESA LIPUMBA
Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye ni Mwenyekiti wa CUF na
Mjumbe wa Bunge hilo, alisema kinachopiganiwa na Ukawa siyo katiba ya chama
chochote cha siasa, bali ya wananchi, hivyo akasema wataendelea kuidai na kudai
pia kutekelezwa matakwa yao.
Alisema Ukawa inaunga mkono kauli ya Mbowe na viongozi
wengine wa umoja huo kuhusu umuhimu wa wafuasi wa Ukawa kuungana siyo katika
kudai tu katiba ya wananchi, bali pia katika kupata serikali imara mwakani.
ISMAIL JUSSA LADHU
Mjumbe wa Bunge hilo, ambaye ni Mwakilishi wa Mjimkongwe
(CUF), Ismail Jussa Ladhu, alisema kwa miaka mingi Wazanzibari wamekuwa
wakiwashuhudia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar wakiwa kitu kimoja,
lakini walipofika Dodoma wakashuhudiwa wakiufyatana kuhoji sababu za ukali wao
kuishia katika baraza hilo.
Alisema alichogundua ni kuwa kinachowasumbua watu hao ni
matumbo yao badala ya maslahi ya Wazanzibari.
Aliwataka Wazanzibari kuhakikisha wanalipiza kisasi
dhidi ya usaliti unaodaiwa kufanywa na watu hao aliowaita kuwa ni wasaliti na
wanafiki.
Alisema inasikitisha kuona leo haki za Wazanzibari
zinatetewa na wananchi wa Tanzania Bara, kama Lissu, Mnyika na Mbatia, badala
ya Wazanzibari wenyewe.
MOSENA NYAMBABE
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, ambaye ni mmoja wa viongozi
wa Ukawa nje ya Bunge, Mosena Nyambabe, alisema fursa ya kutunga katiba mpya ni
fursa ambayo tangu kupatikana kwa uhuru Watanzania hawajawahi kushirikishwa
katika hilo.
Hivyo, alisema daima hawako tayari kukubali CCM
kuwarudisha kwenye katiba ya zamani baada ya kuikarabatina kuiwekea viraka,
bali wanachokitaka ni katiba mpya.
DK. WILLIBROD SLAA
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alisema Watanzania wanasubiri matokeo ya mkutano
wa leo baada ya Ukawa Nje ya Bunge kuzunguka mikoa kadhaa hadi vijijini, ambako
kote alisema hawana chaguo linguine zaidi ya kutaka serikali tatu.
Alisema madai kwamba, waliozaliwa baada ya mwaka 1964
hawaijui Zanzibar ni ya upotoshaji mkubwa.
Dk. Slaa pia alisema pia madai kwamba, zikipitishwa
serikali tatu jeshi litachukua nchi, halina msingi kwa kuwa kuna fedha, ambazo
ni mishahara na posho za wanajeshi zilikatwa, lakini hawakupindua serikali.
DK. MAKAIDI
Mwenyekiti wa NLD, ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge hilo, Dk. Emmanuel
Makaidi, alisema katika serikali tatu kuna imani tatu; ya wananchi, ya Mungu na
uzalendo, lakini hakuna imani yoyote.
MCHUNGAJI MTIKILA
Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye pia Mjumbe wa
Bunge hilo, alisema Zanzibar walitangulia kupata akili tofauti na wenzao
Watanganyika.
TUNDU LISSU
Mjumbe Tundu Lissu alisema kwa nusu karne Zanzibar
haijawa huru, badala yake imekuwa koloni la Tanganyika.
Alisema hali hiyo inatokana na masuala yote ya Zanzibar
ya mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa, ulinzi, uchumi, fedha, sarafu,
mabenki na benki kuu, kwa miaka yote hiyo kuendelea kuamuliwa jijini Dar es
Salaam.
Alisema Zanzibar haiku huru, basi na Tanganyika nayo pia
haiwezi kuwa huru kwa kuwa hakuna mahali popote katika kumbukumbu za serikali
kuna jina Tanganyika na kusema kuwa Watanganyika wameamua kukana uwapo wa
Tanganyika ili waendelee kuikalia Zanzibar.
“Bila Zanzibar huru Tanganyikahaiwezi kuwa huru,”
alisema Lissu.
Alisema makubaliano ya Muungano hayakuua nchi hizo
mbili, hivyo akasema madai kwamba, kuna nchi moja ni uwongo.
Lissu alisema baada ya nusu karne ya kutawaliwa
Wazanzibari wameamka, wanataka Zanzibar huru yenye mamlaka kamili, itawakomboa
pia Watanganyika kwa kuwa wote watakuwa wote huru na hivyo, watakuwa wanafanya
mambo kwa misingi ya haki sawa, tofauti na sasa.
“Umefika wakati wa kupata mamlaka kamili ya Zanzibar ili
kuwatoa Watanganyika mafichoni,” alisema Lissu.
Aliwaomba Wazanzibari wawaongoze tena Watanganyika kile
walichowaongoza miaka 30 iliyopita wakati wa harakati za Mapinduzi yaliyoung’oa
madarakani utawala wa kisultani visiwani humo.
Alisema hiyo ni kwa kila Mzanzibari kuhakikisha anamkaba
rafiki, jirani na mbunge wake, ambaye ni mjumbe wa Bunge hilo kuhakikisha
Zanzibar huru inapatikana.
PROF. ABDUL SHARIF
Mjumbe wa Bunge hilo, Profesa Abdul Sharif, aliwataka
wananchi kuwa pamoja akisema ndiyo njia pekee ya kufikia mafanikio ya kile
wanachokitafuta katika mchakato wa kupata katiba mpya iliyobora.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment