Waziri wa Fedha Saada Salum Mkuya |
SERIKALI imepanga kutumia Sh trilioni 19. 7 katika mwaka
wa fedha 2014/2015, kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo, tofauti na
Sh trilioni 18.2 ya mwaka huu wa fedha unaoishia Juni 30.
Katika fedha hizo, matumizi ya kawaida yamepangwa kuwa
Sh trilioni 14.2, ambapo kati ya hizo Sh trilioni 5.1 ni kwa ajili ya mishahara
ya watumishi wa Serikali, taasisi na wakala wake.
Aidha Sh trilioni 4.4 zimetengwa kwa ajili ya Mfuko Mkuu
wa Serikali na Sh trilioni 4.4 kwa ajili ya matumizi mengine. Waziri wa Fedha,
Saada Salum Mkuya alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akiwasilisha Mpango wa
Bajeti ya mwaka ujao wa fedha kwa wabunge.
MATUMIZI YA MAENDELEO
Alisema makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa mwaka
ujao wa fedha ni Sh trilioni 7.7 sawa na asilimia 39.3 ya matumizi yote ya
Serikali na kati ya kiasi hicho, miradi ya maendeleo imetengewa Sh trilioni 5.4
sawa na asilimia 27.7 ya matumizi yote ya Serikali, huku matumizi mengine ya
maendeleo yakitengewa Sh trilioni 2.2.
“Kwa upande wa matumzi mengine ya maendeleo, a s i limia
63 inagharimiwa na fedha za ndani hivyo kuongeza kujitegemea,” alisema.
Alisema katika matumizi mengine ya maendeleo Sh bilioni
751.7 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara, Sh trilioni 1.4
zimetengwa kwa ajili ya malipo ya mikopo iliyokopwa na makusanyo ya Halmashauri
ya Sh bilioni 138.7, yatatumika kwa ajili ya maendeleo.
VIPAUMBELE
Kwa mujibu wa Waziri Mkuya, katika matumizi ya
maendeleo, Bajeti itazingatia kutekeleza Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza
Umasikini (Mkukuta II), Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano 2011/2012 mpaka
2015/2016 na Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Katika BRN, Waziri Mkuya alisema Bajeti itajielekeza
katika maeneo sita ya kitaifa ambayo ni kilimo, elimu, maji, utafutaji
rasilimali fedha, nishati na uchukuzi na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji
biashara.
KILIMO
Katika Kilimo, Serikali inapanga kuhamasisha kilimo cha
kibiashara cha ngano na miwa ya kuzalisha sukari katika Mto Wami, Ruvu, Kagera,
Kilombero na Malagarasi.
Pia inalenga kuboresha skimu za masoko na umwagiliaji wa
mpunga kwa ajili ya wakulima wadogo, kujenga skimu za pamoja kwa ajili ya
kuwaunganisha wakulima wa mahindi na masoko na kuongeza upatikanaji na utumiaji
wa pembejeo, zana za kilimo na huduma za ugani.
ELIMU
Serikali katika elimu, imepanga kuweka mkazo katika
maeneo yaliyokubaliwa kutekelezwa chini ya BRN, ambayo hata hivyo
hayakufafanuliwa.
MAJI
Waziri Mkuya alisema katika sekta ya maji, Serikali
inapanga kuwezesha kudumu kwa miradi iliyopo ya maji kwa kuhakikisha jamii
inashirikishwa ipasavyo katika kuisimamia.
Pia Serikali imepanga kuongeza vituo vya upatikanaji
maji vijijini kwa kupanua, kukarabati pamoja na kujenga vituo vipya vya
usambazaji maji.
Malengo mengine ya kipaumbele ni kuendelea na
utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maji ikiwa ni pamoja na Kimbiji, Mpera na
bwawa la Kidunda na kuboresha miradi ya usambazaji maji safi na taka katika
maeneo ya mijini.
MADINI
Katika sekta ya madini, msisitizo uliwekwa katika
kuhakikisha Serikali inapata mapato ya kutosha kutoka sekta ya madini kwa
kuzijengea uwezo ofisi za kanda na kuhamasisha uongezwaji wa thamani wa madini
ili kuongeza ukusanyaji wa mapato.
MIUNDOMBINU
Sekta ya miundombinu katika malengo hayo ya kipaumbele,
imegawanywa katika makundi sita ambayo ni reli, barabara, madaraja na maghati,
bandari na usafiri wa majini, usafiri wa anga, utabiri wa hali ya hewa na
nishati.
Katika nishati, Serikali imelenga kukamilisha ujenzi wa
bomba la gesi asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam na kuendeleza
utekelezaji wa miradi mingine 28 ya umeme chini ya mfumo wa BRN.
Pia Serikali imelenga kuendelea kuimarisha miundombinu
ya uzalishaji nishati ya umeme iliyopo pamoja na kupeleka umeme vijijini na
kuhamasisha uwekezaji katika nishati jadidifu.
Katika eneo hilo la miundombinu, Serikali imejipanga
kuboresha miundombinu ya utabiri wa hali ya hewa pamoja na kujenga uwezo wa
watumishi na taasisi ya utabiri wa hali ya hewa.
Katika eneo la usafiri wa anga, Serikali imepanga
kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga, kujenga viwanja vya ndege katika
maeneo ya kimkakati pamoja na kukarabati vilivyopo na kuboresha mazingira ya
kibiashara ilikuvutia wawekezaji.
RELI, BARABARA, BANDARI
Kuhusu reli, Serikali imejipanga kuweka mkazo katika
kuendelea kuimarisha Reli ya Kati, kukarabati na kutengeneza reli zilizopo,
ununuzi wa vichwa vya treni, mabehewa na vifaa vingine.
Pia Serikali imejipanga kukarabati na kutengeneza mifumo
ya mawasiliano ya simu pamoja na mfumo wa ufuatiliaji wa mizigo na kuendelea na
utekelezaji wa miradi mipya ya reli katika maeneo ya kimkakati.
Kwa upande wa barabara, Serikali imejipanga kujenga na
kukarabati barabara zinazofungua fursa za kiuchumi pamoja na kupunguza foleni
katika maeneo ya mijini, kujenga na kuimarisha mizani, kutekeleza miradi
mingine 23 ya barabara iliyoainishwa chini ya mfumo wa BRN na kuendeleza na
kuimarisha barabara zinazounganisha mikoa, wilaya na vijiji, kujenga madaraja,
maghati na ununuzi wa vivuko.
Katika bandari, Serikali imejielekeza kujenga bandari
mpya katika maeneo ya kimkakati pamoja na kuimarisha zilizopo, kuongeza uwezo
wa kubeba mizigo katika bahari, maziwa na bandari kavu na kuongeza ufanisi wa
utendaji kazi katika bandari na kuweka mazingira stahiki kwa ajili ya sekta
binafsi kuwekeza.
Kipaumbele cha sita katika mfumo wa BRN,
kitakachozingatiwa na Bajeti ijayo, ni utafutaji wa rasilimali fedha, ambapo
Serikali imejipanga kupanua wigo wa ukusanyaji kodi ikiwa ni pamoja na
kuimarisha ukusanyaji wa ushuru wa forodha.
Pia Serikali imejielekeza kuimarisha ukusanyaji wa
mapato yasiyo ya kodi, kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya ubia kati ya
Serikali na sekta binafsi, pamoja na kuanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya
kuwezesha ubia kati ya serikali na sekta binafsi.
Serikali pia imejipanga kuanzisha mfuko maalumu kwa
ajili ya kuwezesha ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, kuhimiza malipo kwa
njia ya mtandao na kupunguza misamaha ya kodi.
MAPATO
Waziri Mkuya alisema sera ya mapato kwa mwaka 2014/2015,
inalenga kuimarisha utaratibu wa kukusanya mapato pamoja na kudhibiti na
kupunguza misamaha ya kodi hadi asilimia moja ya Pato la Taifa.
Serikali pia imepanga kukamilisha utungwaji wa sheria ya
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kuongeza wigo wa kodi kwa kuimarisha vyanzo
vilivyopo na kuainisha vyanzo vipya pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi,
ili iingie kwenye mfumo rasmi wa kodi.
“Serikali imekamilisha utafiti wa mfumo wa ukusanyaji wa
mapato yasiyo ya kodi ambapo utafiti umelenga kuhuisha na kuwianisha mifumo ya
ukusanyaji wa mapato hayo ambapo matokeo yake yatajumuishwa katika maboresho ya
mfumo wa kodi kwa mwaka huu,” alisema.
CHANZO: Habari leo
0 comments:
Post a Comment