Kiongozi wa upinzani nchini Malawi, Peter Mutharika,
ametangazwa kuwa mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi wa Mei 20 baada ya
Mahakama Kuu nchini humo kuruhusu utoaji wa matokeo.
Tume ya uchaguzi nchini humo imemtangaza bwana
Mutharika, ambaye ni kiongozi wa chama cha Democratic Progressive Party (DPP), kuwa
ameshinda kwa asilimia 36.4.
Mgombea wa chama cha kihafidhina, Lazarus Chakwera,
ameshika nafasi ya pili akiwa na asilimia 27.8 ya kura huku Rais anayeondoka
madarakani Joyce Banda akishika nafasi ya tatu kwa asilimia 20.2.
Matokeo hayo yametangazwa muda mfupi baada ya mahakama
kuu kutupilia mbali ombi la kutaka kucheleweshwa kwa utoaji wa matokeo ya
uchaguzi huo. Mahakama hiyo pia ilikataa ombi la kutaka kura zihesabiwe upya
kwa mikono pamoja na wito wa kutaka uchaguzi huo urudiwe.
Kabla ya uamuzi huo wa mahakama, mtu mmoja alipoteza
maisha kusini mashariki mwa mji wa Mangochi baada ya polisi kufyatua gesi ya
kutoa machozi na risasi za mpira dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakitaka kura
zihesabiwe upya.
Wito wa kutaka kura zihesabiwe upya ulianza kutolewa na
chama cha Malawi Congress Party (MCP) cha rais wa zamani wa nchi hiyo Kamuzu
Banda baada ya matokeo ya awali kuonesha mgombea wao, Chakwera, akiwa katika
nafasi ya pili.
Aidha, Rais Banda alikuwa ametangaza kufuta matokeo ya
uchaguzi na kutangaza kurudiwa kwa uchaguzi kwa madai kuwa tume ya uchaguzi
ilikuwa imegubikwa na kasoro nyingi ikiwemo kushindwa kukagua rajisi ya wapiga
kura katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.
Hata hivyo, mahakama kuu ilifutilia mbali uamuzi wa
Banda ikisema kuwa rais hana mamlaka ya kubatilisha uchaguzi.
Wakati hayo yakijiri, taarifa zilizoifikia Mzizima24
hivi punde zinasema kuwa Bi Joyce Banda amemtaka radhi bwana Peter Mutharika na
kumuomba nafasi ya kujiunga na chama chake cha DPP baada ya kutangaza kukivunja
chama chake.
0 comments:
Post a Comment