WEZI wameruka ukuta wa makazi ya Mkuu wa Wilaya ya
Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga, kuvunja banda la kufugia na kuchukua mifugo
yote iliyokuwemo. Katika tukio hilo la juzi kuku wote waliokuwa kwenye banda
hilo lililojengwa kwa matofali waliibwa.
Polisi wamesema kwamba baada ya kuingia katika makazi
hayo wezi hao walitoboa ukuta wa chumba ambacho kuku hao walihifadhiwa na
kuwaiba.
Idadi ya kuku walioibwa haikuweza kujulikana mara moja
na Mkuu wa Wilaya amesema atatoa taarifa baada ya kupata maelezo kamili ya
Jeshi la Polisi nini kilitokea katika makazi hayo.
“Ni tukio ambalo linatuumiza sana kichwa kwa eneo kama
hili kuvamiwa na kuvunjwa,” alisema.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari
hizi, baadhi ya wakzi wa mji wa Mbinga wamesema ni jambo la kushangaza kwa eneo
hilo kuvamiwa na wezi, hivyo ni vyema ulinzi ukaimarishwa ili matukio kama haya
yasiweze kuendelea kuwepo.
“Mkuu wa Wilaya ni mwakilishi wa Rais wetu inakuwaje
eneo la Ikulu ndogo kama ile ambapo anaishi panavamiwa na wezi, wakati vyombo
vya usalama vipo, vinafanya kazi gani”, alihoji mmoja wa wananchi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Deusdedith Nsimeki
alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo.
“Ni kweli taarifa juu ya kuvamiwa na kuvunjwa banda la
kufugia kuku katika eneo hilo nimezipata hivi punde, kuku kadhaa wameibwa.
”Idadi yake bado sijaipata lakini uchunguzi bado
unaendelea ili tuweze kubaini nani aliyehusika na uhalifu huo, kwa hivi sasa
hakuna mtu tunayemshikilia,” alisema Kamanda.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa Wilaya
alisema kikubwa kinachomsikitisha zaidi, ni kwamba hapo nyumbani kwake ni Ikulu
ndogo; Ni jengo la Serikali na walinzi wanaoshiriki ni askari Polisi na
walikuwa na silaha.
0 comments:
Post a Comment