Zaidi ya watu 40 wamepoteza maisha na wengine wapatao 80 kujeruhiwa katika mashambulizi ya mabomu nchini Iraq, hususan katika mji mkuu Baghdad,
Leo Jumatatu, mashambulizi mfululizo ya mabomu -hasa yaliyotegwa kwenye magari - yamewaua watu 30 na kuwajeruhi wengine wapatao 70 mjini Baghdad.
Polisi wanasema kuwa kwa uchache milipuko saba ilitokea katika wilaya mbalimbali kama vile Zafaraniyah, Alam, Obeidi, Dora, Sadiyah, Kam Sarah na al-Jadidah.
Mapema leo, milipuko kadhaa iliua zaidi ya dazeni ya watu katika miji mbalimbali nchini Iraq kama vile Fallujah na Baquba. Mashambulizi hayo pia yaliwajeruhi zaidi ya watu 15.
Siku za Jumamosi na Jumapili, mfululizo wa mashambulizi ya mabomu uligharimu maisha ya watu 105, wakiwemo watoto, na kuwajeruhi zaidi ya watu mia moja mjini Baghdad na katika kijiji cha Qabak kilichopo kazikazini mwa mji huo.
Mpaka sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na milipuko hiyo, huku baadhi ya watu wakiyahusisha matukio hayo na makundi ya wapiganaji wenye uhusiano na al-Qaeda, ambao inasemekana kuwa lengo lao ni kuiyumbisha serikali kuu.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu wapatao 1,000 walipoteza maisha na zaidi ya 2,000 kujeruhiwa katika ghasia zilizotokea nchini Iraq mwezi Septemba, na kuufanya mwezi huo kuwa miongoni mwa miezi mibaya kabisa katika miaka ya hivi karibuni
Wizara ya Mambo ya Ndani imesema kuwa wanamgambo wameanzisha vita ya wazi nchini Iraq na wanataka kuitumbukiza nchi hiyo ya Kiarabu katika machafuko.
0 comments:
Post a Comment