SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuvisihi vyama
vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kusitisha maandamano yao na kurejea meza ya
mazungumzo ili kupata muafaka wa muswada wa sheria ya kubadili sheria ya mabadiliko
ya katiba, vyama hivyo vimetoa masharti mazito ya kukutana naye.
Hatua hiyo inakuja wakati vyama hivyo vikiendelea
kushikilia msimamo wao wa kuitisha maandamano ya nchi nzima kupinga muswada
huo, wanaodai kuwa unalenga kuipa CCM nafasi ya kuhodhi mchakato wa katiba
mpya.
Wakati vyama hivyo vikiwa vimefanya mikutano ya ndani na
makundi mbalimbali, na kisha mikutano miwili ya hadhara Dar es Salaam na
Zanzibar, CCM nayo inakazana kumshinikiza rais asaini muswada huo kama
ulivyopitishwa na Bunge.
Inasemekana kuwa kuna mvutano mkali ndani ya CCM, ambako
makundi ya vigogo wanaotajwa kugombea urais mwaka 2015, wanampinga Rais Kikwete
kwa jinsi anavyoendesha mchakato huo, wakidai anawabeba wapinzani.
Licha ya wadadisi wa masuala ya kisiasa kumtabiria Rais
Kikwete kuwa anaweza kujiandikia historia nzuri endapo mchakato huo ukifanikiwa
kwa kuzingatia matakwa ya wananchi, CCM inamtazama mwenyekiti huyo kama anataka
kuwakomoa wenzake.
“Kuna msuguano mkali ndani ya CCM, Rais Kikwete ana nia
njema na mchakato huu ili ukamilike kwa amani, lakini wenzake ndani ya chama
wanadhani anataka kuwanufaisha wapinzani kwani hatakuwa na chochote cha
kupoteza,” alisema kigogo mmoja wa CCM.
Ni katika nia njema hiyo Rais Kikwete katika hotuba yake
ya mwisho wa mwezi, aliwasihi viongozi wa vyama vitatu vya upinzani
kutoandamana, badala yake wakae na kutafuta njia mbadala ya kisheria kuboresha
muswada huo, na kwamba serikali iko tayari kuwasikiliza.
Hata hivyo, wito wa Rais Kikwete umepokelewa kwa taswira
tofauti na vyama hivyo, vikisema kuwa yeye ndiye anapaswa kuwaandikia barua
kuwaomba akutane nao kwa mazungumzo Ikulu, kwani wao hawajawahi kuomba kukutana
naye.
Badala yake, vyama hivyo vilisisitiza kuwa viliomba
kukutana na wadau mbalimbali na wananchi kumshinikiza asisaini muswada, na
kwamba msimamo wao uko pale pale.
Katika msimamo huo, vyama hivyo vimesema maandamano
yaliyotangazwa kufanyika Oktoba 10 nchi nzima yako pale pale, na kamati ya
maandalizi inaendelea kufanya taratibu zote.
Wakizungumza jana jijini Dar es Salaam, wawakilishi wa
vyama hivyo, John Mnyika (CHADEMA), Faustine Sungura (NCCR-Mageuzi) na Abdul
Kambaya (CUF), walisema kuwa kamati ya maandalizi ya maandamano inaendelea kwa
kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake hakugusia suala lolote kama atasaini
muswada huo au la.
“Rais amezungumzia hoja za upinzani za kuvunjwa kwa Tume
ya Jaji Joseph Warioba kabla ya kumaliza muda wake, kwa hili tunampongeza,
amekuwa wazi. Lakini afahamu kuwa hiyo si hoja kuu iliyosababisha tuandae
maandamano kushinikiza asisaini huo muswada.
“Mambo mengine mazito yapo, kuhusu muundo wa Bunge la
Katiba na idadi ya wajumbe kwa uwiano sawa wa Zanzibar na Tanganyika na kuhusu
maoni ya wadau kuachwa,” alisema Mnyika.
Alisema kuwa maoni ya wadau yamepuuzwa, uchakachuaji
umefanyika, taasisi zilipeleka majina, lakini Rais Kikwete anasema kuwa
alizingatia hilo, kwamba wanamwomba aseme kwanini hakuchukua jina kati ya yale
yaliyopendekezwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Shirikisho la
Vyama vya Wenye Ulemavu (Shiwavyata) na CCT.
Alisema kuwa hao walijitokeza kwenye kamati wala hawakusema
kwa siri, hivyo Rais Kikwete awaambie mawaziri wake wamwambie ukweli.
Alihoji kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake ametumia
neno ‘nimeambiwa’ kwa kiasi kikubwa, kwamba ingefaa mawaziri wake hasa Waziri
wa Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi; Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias
Chikawe; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira na
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba wamwambie ukweli.
“Huyu huyu rais ndie aliwaambia wafanyakazi wakati wa
mgomo wao kuwa akili za kuambiwa na viongozi wao wachanganye na za kwao,
kwanini katika mambo aliyoambiwa na wasaidizi wake hakujiridhisha kwanza?”
alihoji.
Hivi karibuni, Waziri Wassira aliwakejeli wapinzani kuwa
wasitarajie tena kukaribishwa Ikulu, kutokana na msimamo wao wa kususia mjadala
wa muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013.
Alisema kuwa maandamano yaliyokuwa yanaandaliwa
kumshinikiza rais asisaini muswada huo, hayana maana kwani rais hana sababu za
kutousaini.
Licha ya Wassira kudai milango ya wapinzani kuzungumza
na rais katika suala hilo imefungwa, Rais Kikwete amewasihi wapinzani wakae na
serikali wajadili kasoro zilizopo kwenye muswada kama walivyofanya mwaka 2011
wakati mchakato unaanza hatua ya kwanza.
Hata Waziri Chikawe naye alimtisha rais hivi karibuni
kuwa iwapo ataliafiki suala hilo la wapinzani na makundi mengine, na kuacha
kutia saini muswada huo, atakuwa ametengeneza mgogoro na mhimili wa Bunge kutokana
na chombo hicho kukamilisha kazi yake.
Lakini rais amewapuuza mawaziri wake hao na kutumia
busara akisema kuhusu hoja ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kutokufanya
vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau, saula hilo lilianzia bungeni hivyo linaweza
kurudishwa huko lijadiliwe tena.
Kuhusu rais kumwandama Msemaji wa Kambi ya Upinzani,
Tundu Lissu kuwa alisema uongo bungeni, Mnyika alisema hakufanya vema
kumshambulia mbunge huyo kwani hayo hayakuwa mawazo yake binafsi bali maoni ya
kambi ya upinzani.
“Inakuwa sio vizuri mbunge aliyetoa mawazo bungeni kwa
mujibu wa katiba na kanuni za Bunge kushambuliwa kwa maneno makali na rais
wakati alikuwa anatoa mawazo ya kambi wala si yake,” alisema Mnyika.
0 comments:
Post a Comment