Serikali imetangaza kuifanyia matengenezo makubwa meli
kongwe nchini yenye miaka 100 ikitoa huduma MV LIEMBA katika Ziwa Tanganyika
mkoani Kigoma. Na imefuta mpango wa kuifanya meli hiyo makumbusho kama ambavyo
mashauriano ya Tanzania na Serikali ya Ujerumani yalivyokuwa yameelekeza.
Meneja wa Kampuni ya huduma za Meli mkoa wa Kigoma Abel
Gilliard amekaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa badala ya meli hiyo
kufanywa kuwa sehemu ya makumbusho kwa utalii, sasa meli hiyo itafanyiwa
matengenezo makubwa ili iendelee kutoa huduma za usafirishaji wa watu na mizigo
katika Ziwa Tanganyika baina ya bandari ya Kigoma na Mpulungu nchini Zambia.
Serikali tayari imetiliana saini ya mkataba na kampuni
ya Diak Techinical Export ya jimbo la Southampton nchini Uingereza ambapo meli
hiyo itafanyiwa matengenezo hususani katika injini yake, vifaa vya kuongozea
meli na baada ya matengenezo hayo kukamilika mwishoni mwa mwaka 2014 yataifanya
meli hiyo kudumu kwa miaka 30 mingine ijayo.
Awali Serikali ya Ujerumani ilitaka kuichukua meli hiyo
na kuifanya kivutio cha utalii ma kuleta meli nyingine mbili ahadi ambayo
imeonekana kutotimizwa na hivyo Serikali kuachana na mpango huo.
MV Liemba zamani ikiitwa "Graf Goetzen"
ilitengenezwa mwaka 1913 na kampuni ya Kaiserliche Marine ya nchini Ujerumani
na kutumiwa na jeshi la Ujerumani enzi za ukoloni, ni meli pekee iliyokatika
rekodi za ulimwengu kama meli kongwe ya abiria na mizigo ambayo bado inaendelea
kutoa huduma.
Meli hii iliwahi kutumika kama meli ya kivita wakati wa
vita ya kwanza ya dunia na Ujerumani ikaizamisha mwaka 1916 (katika ghuba ya
Katabe ambayo leo inaitwa Bangwe) wakati majeshi yake yalipozidiwa na vikosi
vya Uingereza na kulazimika kutoroka. Mwaka 1924 Serikali ya Uingereza iliibua
tena meli hii ikapewa jina la S.S Liemba na mwaka 1927 ikaanza tena kutoa
huduma za usafirishaji abiria na mizigo mpaka leo hii.
MV Liemba ni utambulisho wa Tanganyika na jina lake
Liemba ni jina la asili ya wenyeji wa Kigoma.
0 comments:
Post a Comment