TUKIO lililotokea nchini Kenya katika jengo la biashara
la Westgate, limeizindua Tanzania na hivyo wamiliki wa majengo makubwa ya
biashara likiwemo Mlimani City jijini Dar es Saalam kuimarsha ulinzi.
Tangu kutokea kwa tukio hilo linalodaiwa kutekelezwa na
kundi la Al-Shabaab la nchini Somalia na kusababisha vifo vya watu 67 na
wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa, nchi za Afrika Mashariki zimeanza kuchukua
tahadhari kubwa katika kukabiliana na vitendo hivyo.
Jana ulishuhudiwa msafara mkubwa wa magari uliokuwa
ukiingia katika jengo lenye maduka mbalimbali ya biashara la Mlimani City
yakifanyiwa upekuzi wa kina, huku madereva wakitakiwa kuteremka na kuyaacha
tupu.
Aidha, baadhi ya wafanyakazi wa jengo hilo waliovalia
vifaa maalumu walikuwa wakivipitisha chini ya magari yaliyoingia katika jengo
hilo kwa umakini wa hali ya juu tofauti na siku za nyuma ambazo watu waliingia
na kutoka bila kukaguliwa.
Mmoja wa kiongozi wa ukaguzi huo ambaye ni raia wa
kigeni, alionekana kuwa makini na kuwataka wateja wote walioingia na magari yao
ndani ya eneo hilo kuyaweka pembeni ili yafanyiwe upekuzi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mmoja wa
madereva, Juliaus Janco alisema kuwa ni vyema utaratibu huo ukawekwa katika
kila jengo lenye msongamano wa watu ili kukabiliana na maafa yanayoweza
kutokea, hasa katika kipindi hiki cha uwepo wa magaidi.
Alisema kuwa pamoja na baadhi kuonekana kukerwa na
utaratibu huo, lakini wanapaswa kuelewa kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza
hofu iliyojengeka sasa, hasa watu wanapoingia katika majengo kama hayo.
Katika hotuba yake ya juzi, Rais Jakaya Kikwete pia
aligusia tukio hilo la kigaidi la Kenya akisema kuwa anafahamu kuwa baada ya
tukio hilo watu wengi nchini wameingiwa na hofu kuhusu usalama.
“Ni hofu ya msingi kwani Agosti 8, 1998, Ubalozi wa
Marekani hapa nchini ulishambuliwa na magaidi na ndugu zetu 11 wasio na hatia
walipoteza maisha,” alisema.
Alisema kuwa tangu shambulio la mwaka 1998, serikali
imekuwa inajenga uwezo wa vyombo vya ulinzi na usalama kupambana na ugaidi
katika nyanja mbalimbali.
“Tunaendelea kujiimarisha bila kusita siku hadi siku.
JWTZ, Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa
ajili hiyo. Juhudi zetu hizo ndizo zinazotufanya tuwe salama hadi sasa,”
alisema.
Rais aliongeza kuwa baada ya tukio la Kenya, vyombo vya
ulinzi na usalama vimeimarisha mikakati yao maradufu. Kwamba pamoja na
kujizatiti hawawezi kusema kuwa tukio la kigaidi halitaweza kutokea nchini.
“Uhakika huo hatuna kwani hata mataifa makubwa na tajiri
yameshambuliwa. Kilicho muhimu ni kuendelea kuchukua tahadhari na wananchi
kusaidia ili vyombo vyetu vifanikiwe zaidi.
“Hali kadhalika, tumewataka watu wote wenye shughuli
zinazokusanya watu wengi kama vile maduka, maofisi, mahoteli, migahawa waweke
kamera za ulinzi nje na ndani ya maeneo yao,” alisema.
Pia aliwataka waangalie uwezekano wa kuweka vifaa vya upekuzi
(metal detectors and x-rays). Kwamba anajua watu wanaweza kulalamikia usumbufu
au gharama, lakini gharama na hasara ya kushambuliwa ni kubwa zaidi kuliko ya
usumbufu huo.
KENYA YATAJA WATUHUMIWA UGAIDI
Wakati huohuo, habari kutoka Nairobi, Kenya zinasema
kuwa nchi hiyo imetoa majina ya watu wanne ambao inasemekana walifanya
shambulio dhidi ya jengo la maduka la Westgate wiki mbili zilizopita.
Watu ambao wote ni wanaume, walionekana kwenye picha za
kamera za usalama zilizopatikana Westgate baada ya jengo hilo kushikiliwa na
Al-Shabaab kwa siku nne.
Msemaji wa jeshi aliwataja watu hao kuwa ni Abu Baara
al-Sudani, Omar Nabhan, Khattab al-Kene na Umayr.
Taarifa zinasema kuwa wawili kati yao wana uhusiano na
al-Qaeda na mmoja ana uhusiano na wapiganai wa al-Shabaab ambao walikiri
kuhusika na shambulio la Westgate.
0 comments:
Post a Comment