WANAHARAKATI wanawake nchini Saudi Arabia wameweka picha
na video mbalimbali kwenye mtandao wa intaneti zikiwaonesha wakiendesha magari,
ikiwa ni hatua ya kupinga marufuku ya wanawake kutoendesha magari iliyowekwa na
utawala wa nchi hiyo.
Picha na video hizo zilizoanza kuwekwa jana Alhamisi,
ziliwaonesha wanawake mbalimbali wa Kisaudi wakiendesha magari katika mji mkuu
wa nchi hiyo, Riyadh.
Mwanaharakati mmoja wa Kisaudi, aliyezungumza kwa sharti
la kutotajwa jina, alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kampeni yenye hatua
mbili inayolenga kupinga marufuku iliyowekwa dhidi ya wanawake kutoendesha
gari. Katika hatua ya pili, wanawake wenye leseni za udereva za kimataifa
watatakiwa kuendesha magari Oktoba 26.
“Kuendesha ukiwa na leseni haipaswi kuchukuliwa kuwa ni kinyume
na sheria,” alisema na kuongeza kuwa, “mamlaka, nchi, fikra za watu
zimebadilika.”
Kampeni hiyo ilizinduliwa baada ya Baraza la Shura la
Saudi Arabia kulikataa ombi la pamoja lililotolewa na wanabaraza wa kike
waliotaka kujadiliwa suala la kuiondosha marufuku hiyo.
Uamuzi huo wa baraza ulikuja licha ya kuongezeka kwa
taarifa na ripoti mbalimbali za wanawake walioamua kuendesha magari katika
kuipinga marufuku hiyo.
Baadaye mwezi huu, wanaharakati wa Kisaudi wanapanga
kufanya maandamano nchi nzima kupinga marufuku hiyo.
Saudi Arabia ndiyo nchi pekee duniani ambayo wanawake
wamepigwa marufuku kuendesha gari. Mwanamke akiendesha gari anaweza kukamatwa,
akapelekwa mahakamani na hata kuchapwa viboko.
Wanaounga mkono marufuku hiyo wanasema kuwa kuwaruhusu
wanawake kuendesha magari ni tishio kwa maadili ya umma na kunawahamasisha na
kuwashawishi kuchanganyika sana na wanaume hadharani.
Mwaka 2011, wanawake kadhaa walishiriki katika kampeni
kama hiyo, waliyoiita: NI HAKI YANGU KUENDESHA, wakipinga marufuku hiyo. Waliweka
picha na video mbalimbali mtandaoni zilizowaonesha wakiwa wanaendesha.
Muda mfupi baadaye polisi waliwakamata baadhi ya
wanawake waliokuwa wakiendesha; wawili miongoni mwao walishitakiwa. Hata hivyo,
waliachiwa huru baada ya kulazimishwa kula kiapo cha kutoipinga tena marufuku
hiyo.
0 comments:
Post a Comment