UMOJA wa Afrika umeelezea wasiwasi wake dhidi ya
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ukiitaka kuzifuta kesi za viongozi wa
Kenya.
Wito huo umetolewa wakati wa kikao cha Umoja huo wenye
wanachama 54 kilichofanyika leo katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa. Viongozi
kadhaa wa Kiafrika waliitaka mahakama hiyo kuondosha mashitaka yanayoukabili
uongozi wa Kenya na nchi nyingine wanachama wa Umoja huo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Tedros Adhanom
Ghebreyesus, aliyeongoza kikao cha leo cha Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, alisema
kuwa AU iliwahi kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuahirisha
mashitaka dhidi ya Rais wa Sudan Omar al-Bashir lakini hawakusikiliza. Vilevile
alilaani vikali jinsi mahakama hiyo inavyowanyanyasa viongozi wa Kiafrika na
kuamiliana nao vibaya.
"Namna ambavyo mahaka imekuwa ikifanya kazi,
hususan inavyowatendea vibaya viongozi wa Kiafrika, inaleta wasiwasi,” Ghebreyesus
aliwaambia mawaziri na wajumbe wengine katika mkutano wa ufunguzi, akaongeza
kuwa, "Badala ya kuleta haki na maridhiano…mahakama hiyo imejigeuza kuwa
chombo cha kisiasa. Muamala huu mbaya na wa ukandamizaji haukubaliki kabisa.”
Kwa kiasi kikubwa mkutano huo unajikita katika kujadili
uhusiano wa AU na mahakama ya ICC. Umoja huo unaituhumu mahakama hiyo yenye
makao yake mjini Hague, Uholanzi, kuwa kazi yake imekuwa ni kuwawinda viongozi
wa Kiafrika na kuwashitaki.
Naibu Rais wa Kenya, William Ruto, kwa sasa anakabiliwa
na mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu.
Ruto pamoja na Rais Uhuru Kenyatta wanatuhumiwa
kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, zilizopoteza maisha ya
watu wapatao 1,200.
Kwa uchache viongozi 8 wa Kiafrika wanachunguzwa na
Mahakama hiyo ya ICC.
Kwa sasa ICC inaendesha kesi za uhalifu dhidi ya
binadamu kutoka katika nchi nane za Kiafrika kama vile Sudan, Jamhuri ya
Kdemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda na Kenya.
Kwa muda mrefu Umoja wa Afrika umekuwa ukijaribu
kustawisha utawala wa kidemokrasia barani Afrika, lakini umekuwa ukikwamishwa
na viongozi kadhaa wanaong’ang’ania madaraka.
0 comments:
Post a Comment