Askari wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania akiwa katika majukumu yake huko Darfur, Suadan |
WALINZI wa amani watatu kutoka Senegal wameuawa wakati
msafara wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa uliposhambuliwa katika Jimbo la
Darfur, nchini Sudan.
Ujumbe wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kwa ajili
ya Darfur (UNAMID) ulisema katika taarifa iliyotolewa jana Jumapili kuwa
shambulizi hilo lilifanywa wakati walianda amani walipokuwa wakiusindikiza
msafara wa maji kutoka mji wa El Geneina kwenda ofisi za UN Magharibi mwa
Darfur.
Shambulizi hilo ni la pili kufanyika dhidi ya walinda
amani wa Umoja wa Mataifa katika jimbo hilo ndani ya siku tatu, ambalo, mbali
na vifo hivyo, lilimjeruhi pia askari mmoja kutoka Senegal.
UNAMID iliongeza kuwa washambualiaji walilivizia gari
lililokuwa umbali wa kilometa saba (maili nne).
Katika radiamali juu ya mashambulizi hayo, Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon,
aliitaka serikali ya Sudan kuchukua hatua za lazima dhidi ya hujuma hizo.
“Kwa mara nyingine tena, walinda amani wa UNAMID
wanashambuliwa wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuwasaidia Wasudan
kupata amani Darfur… Hujuma hizi hazikubaliki,” aliongeza mkuu huyo wa UN na
kuiambia serikali ya Sudan kuwawajibisha wahusika.
Mnamo Oktoba 11, mwanajeshi kutoka Zambia aliuawa katika
shambulizi lililofanywa katika mji wa El Fasher, Kaskazini mwa Darfur.
Mwezi Julai, askari saba wa Tanzania na polisi mmoja wa Sierra
Leone waliuawa na wengine 16 kujeruhiwa karibu na mji wa Nyala katika jimbo la Darfur.
Darfur imekuwa katika hali ya ghasia tangu mwaka 2003, baada
ya waasi kushika silaha dhidi ya serikali ya Sudan. Vilevile kumekuwepo na
mapigano ya kikabila katika jimbo hilo. Zaidi ya watu 300,000 wameshauawa
katika mgogoro huo.
0 comments:
Post a Comment