SERIKALI imesema, mwakani inatarajia kuajiri walimu
wapya 27,000 wa shule za msingi na sekondari nchi nzima. Taarifa hiyo ilitolewa
jijini hapa jana na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI),
Kassim Majaliwa (pichani) alipokuwa akifunga mkutano wa wadau wa Mfuko wa
Pensheni wa LAPF.
Alisema kwamba
kitendo cha kuajiriwa kwa walimu hao, kitatoa fursa ya mifuko ya hifadhi ya
jamii nchini, kupata wanachama wengi na hivyo kuendelea kuboresha shughuli na
maisha ya waajiriwa wao.
“Mwakani tunatarajia kuajiri walimu wapatao 27,000 nchi
nzima na hii itakuwa ni fursa nzuri kwa mifuko ya jamii kwani watajiunga katika
mifuko ya jamii iliyopo,” alisema Majaliwa.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa LAPF, Eliud Sanga alisema, kwa
miaka minne mfululizo, mfuko huo umeongoza kwa utunzaji wa hesabu kwa viwango
vya NBAA.
Kwa mujibu wa Sanga, mwaka jana mfuko huo uliandikisha
wanachama 17,840 na kukusanya michango ya Sh bilioni 119.7 wakati mwaka huu,
mfuko unatarajia kukusanya Sh bilioni 163.
Alisema, LAPF inaendelea kuongeza uwekezaji katika
vitega uchumi kwa kuwekeza Sh bilioni 570, ambapo imefanikiwa kupata faida ya
Sh bilioni 48.7.
Naye Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka,
akichangia katika mkutano huo, aliitaka mifuko ya pensheni nchini kushindana
katika utoaji wa mafao bora ili wanachama wa mifuko wafaidike na mafao bora.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi
wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii, Irene Isaka, aliwataka wananchi kujiunga na
uchangiaji wa hiari katika mifuko mingi kadiri wawezavyo, ili utakapofika umri
wa kustaafu wapate mafao bora kuliko mishahara waliyokuwa wakilipwa.
CHANZO: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment