Na Kabuga Kanyegeri
Serikali ya Marekani imefunga baadhi ya shughuli zake;
wafanyakazi 800,000 wa serikali kuu wamepumzishwa, hifadhi za taifa na maeneo
ya makumbusho vimefungwa; na huduma muhimu za kijamii kama vile mikopo ya
nyumba na programu za lishe zimetatizika. Sio hivyo tu, bali hata Rais Obama
ilibidi avunje safari yake ya kuelekea kwenye mkutano wa viongozi wa nchi za
Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki (APEC) uliokuwa ukifanyika mjini
Bali, nchini Indonesia, ambapo alipanga kutangaza mpango wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Marekani na Jumuiya hiyo yenye
wanachama 21.
Kama tujuavyo, Serikali ni mfano wa gari. Pesa ndiyo
mafuta yake. Gari isipojazwa mafuta, haiwezi kutembea. Bunge la ‘Congress’
nchini Marekani ndilo lenye wajibu wa kuijaza mafuta gari hiyo kwa kupitisha
miswada ya bajeti. Mwaka mpya wa bajeti ulianza Jumanne, tarehe 1 Oktoba, na
Bunge halionekani kuwa lipo tayari kupitisha bajeti husika. Matokeo yake,
serikali itashindwa kufanya baadhi ya kazi zake kwa sababu itakuwa
haijaidhinishiwa fedha.
Kwa nini Bunge halijapitisha bajeti hiyo?
Vyama vikuu vya Republican na Democratic vinapingana
kwenye mpango ulioanzishwa na Rais Obama wa kutoa bima ya huduma ya afya kwa
mamilioni ya Wamarekani wa kipato cha chini ambao hawana bima ya afya. Waunge
wa chama cha Republican hawaupendi mpango huo unaojulikana kama “Obamacare”, na
wanakataa kupitisha vifungu ambavyo vinajumuisha fedha za mpango huo. Hivyo,
wanamshinikiza Rais Obama afute mpango huo nao ndipo watakapopitisha bajeti
hiyo. Wabunge wa Democratic katika Bunge la Seneti wanakataa kupitisha bajeti
isiyokuwa na fedha za mpango huo wa “Obamacare”.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, mpango huu wa Obama
ni pigo kwa makampuni makubwa ya kibepari yanayofaidika na kutokuwepo kwa
mpango huo. Hofu ya makampuni hayo ni kukosa nguvu ya kuwanyonya wananchi
wasiokuwa na huduma ya bima ya afya. Hivyo makampuni hayo yameamua kuwatumia
baadhi ya wabunge kuukwamisha mpango huo kwa kuunyima fedha katika bajeti,
baada ya majaribio kadhaa kushindwa kuukwamisha.
Aidha, inaelezwa kuwa mpango huo ni ushindi mkubwa kwa
Obama na utamuweka katika ramani ya historia, hususan ikizingatiwa kuwa
watangulizi wake wengi walishindwa kuupitisha na kuuanzisha. Hivyo, inadhaniwa
kuwa hatua ya wabunge wa Congress inalenga kumnyima Obama nafasi hiyo ya
taadhima ya kijamiii.
Mbali na hivyo, inaonekana pia kwamba juhudi za Rais
Obama za kuufufua uchumi wa Marekani zinaanza kuzaa matunda, baada ya mtikisiko
wa uchumi ulioukumba uchumi wa dunia katika miaka ya hivi karibuni. Hivyo,
kuinyima serikali yake uwezo wa kukopa zaidi ni kujaribu kudunisha juhudi hizo
za Obama.
Vita hivi vya maneno kuhusu bajeti ya Marekani na ukomo
wa uwezo wa serikali kukopa, vinaweza kuwa na athari kubwa na kuleta mshtuko wa
kiuchumi dunia nzima, kwa sababu masoko ya dunia yanategemea uthabiti wa
Marekani. Hili ndilo lililomfanya Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Christine
Lagarde kuonya: “Kusimama kwa serikali ya Marekani ni jambo bay asana, lakini
kushindwa kuongeza uwezo wa ukomo wa kukopa fedha kwa serikali litakuwa jambo
baya zaidi, na linaweza kuumiza na kuuharibu sio tu uchumi wa Marekani, bali
uchumi wa dunia nzima.”
Iwapo hali hii itaendelea kwa siku kadhaa, wafanyakazi
waliopumzishwa watakuwa katika hali ngumu ya kiuchumi na kifedha.
Na iwapo itaendelea kwa wiki kadhaa, mapato ya utalii yatapotea
na wafanyabiashara au wateja wataogopa kutumia fedha zao kwa hofu ya kuendelea
kwa mdororo.
Na iwapo hali hiyo itafuatiwa na serikali kutokuwa na
uwezo wa kulipa madeni, ambapo hilo linaweza kutokea ndani ya mwezi mmoja kama
Bunge halitachukua hatua, basi wawekezaji wa kigeni wataanza kuwa na wasiwasi
kuhusu nguvu na uwezo wa uchumi wa Marekani. Watapoteza imani na uwezo wa
Marekani kulipa madeni, jambo litakaloongeza viwango vya riba kwa wakopeshaji
wa kigeni. Mbaya zaidi, wawekezaji wa kigeni wanaweza kukosa imani ya kununua
dhamana za Marekani.
Ingawa jambo hili linaonekana kuwa vita kali ya kisiasa
baina ya mirengo miwili, lakini hatua ya Congress kushindwa kupitisha bajeti ya
serikali kuu, mbali na kuwaathiri wafanyakazi 800,000, lakini pi itayaathiri
maisha ya kila siku ya mwananchi wa kawaida wa Marekani.
Mara ya mwisho serikali ilisimamisha kazi zake kwa siku
21, kuanzia Desemba 1996 mpaka Januari 1997, na kuugharimu utawala wa Rais Bill
Clinton karibu dola bilioni 2.
Ni muhimu kuashiria hapa kuwa hatua hiyo inaziathiri
baadhi ya sekta, huku sekta muhimu zikiendelea kufanya kazi.
Jambo ambalo liko wazi ni kuwa hivi ni vita vya kisiasa
kwa kutumia silaha ya bajeti, na Rais Obama ameshikilia msimamo wake wa
kuendelea na mpango wake wa bima ya afya kwa watu wa kipato cha chini.
Lakini, je, Rais Obama ataweza kukabiliana vipi na
changamoto hii? Ni kiasi cha kusubiri na kuona mwisho wa vita hivi.
Kwa maoni:
0 comments:
Post a Comment