Kuwait na nchi nyingine zinatarajiwa kuweka utaratibu wa
vipimo vya afya katika “kuwabaini” mashoga wanaoingia katika nchi za Ghuba.
Afisa mmoja mwandamizi, Yousouf Mindkar anasema kuwa pendekezo
la kuweka vifaa maalumu kwenye viwanja vya ndege katika nchi zote za
Ushirikiano wa Ghuba linaandaliwa. Watu watakaobainika kuwa mashoga
hawataruhusiwa kuingia katika nchi husika.
Kamati iliyopewa jukumu la kushughulikia suala hilo
itakaa Novemba 11 kupitia pendekezo hilo.
Akizungumza na gazeti moja la kila siku nchini Kuwait la
Al Rai, mkurugenzi wa afya ya umma kwenye wizara ya afya alisema kuwa wakati
vituo vya afya tayari vina utaratibu wa kufanya vipimo kubaini afya za wale
wanaoingia Kuwait, watachukua hatua kali zaidi zitakazowasaidia kuwabaini
mashoga ambao watazuiliwa Kuwait au nchi yoyote mwanachama wa Ushirikiano wa
nchi za Ghuba.”
Wale wenye umri chini ya miaka 21 wanaoishi Kuwait
wanapokutwa na hatia ya kushiriki vitendo vya ushoga hupewa adhabu ya kifungo
cha miaka mpaka 10 jela. Vitendo vya ushoga vimepigwa marufuku katika nchi za
Ushirikiano wa Ghuba zinazojumuisha Saudi Arabia, Oman na Umoja wa Falme za
Kiarabu.
Mapema wiki hii, Oman ililifungia kwa muda usijulikana
gazeti la The Week, lilituhumiwa kuchapisha makala iliyochukuliwa kuwa
inawatetea mashoga.
Ushoga umepigwa marufuku katika nchi 78 duniani na katika
nchi tano mtu anayekutwa na hatia ya kufanya ushoga adhabu yake ni kifo. Miongoni
mwa nchi hizo ni Iran, Yemen na Saudi Arabia.
0 comments:
Post a Comment