MAHAKAMA kuu nchini Pakistan imempa dhamana kiongozi wa
zamani wa nchi hiyo, Pervez Musharraf, katika kesi inayomkabili ya mauaji ya
kiongozi mmoja wa upinzani wa jimbo la Balochistan.
Wakili wa Musharraf anasema kuwa hatua hiyo itapelekea
kuachiwa huru kutoka katika kizuizi cha nyumbani.
"Pervez Musharraf yuko huru sasa baada ya kupata
dhamana katika kesi ya Bugti,” alinukuliwa wakili Qamar Afzal.
Musharraf alikuwa rais wa Pakistan pindi Akbar Bugti, kiongozi
mkuu katika jimbo la kusini magharibi la Balochistan, alipofariki katika
shambulizi la jeshi Agosti 2006.
Mpaka sasa Musharraf ameshapewa dhamana tatu, ikiwemo
ile ya mauaji ya waziri mkuu wa zamani, Benazir Bhutto.
Kwa sasa yupo katika kizuizi cha nyumbani mjini Islamabad
kuhusiana na kesi kadhaa zinazomkabili, ikiwemo hiyo ya Bhutto.
Bhutto aliuawa katika shambulizi la bomu Desemba 27,
2007, wakati akitoka kwenye mkutano wa kampeni katika mji wa Rawalpindi.
Musharraf anatuhumiwa kwa kushindwa kumpa Bhutto ulinzi wa kutosha baada ya
kutoka uhamishoni Oktoba 18, 2007.
Vilevile anakabiliwa na mashitaka ya kuwaweka katika
kizuizi cha nyumbani majaji kinyume cha sheria baada ya kumtimua Jaji Mkuu Iftikhar
Muhammad Chaudhry, akatangaza hali ya hatari, na kusitisha matumizi ya katiba,
wakati akijaribu kuukandamiza mhimili wa mahakama mwaka 2007.
Aidha, Musharraf anatuhumiwa kukiuika katiba kwa kutoa
amri ya kuwakamata majaji na kuwaweka kizuizini.
Mtawala huyo wa zamani wa kijeshi anakanusha tuhuma hizo
na kudai kuwa zinachochewa kisiasa.
Jenerali huyo wa zamani, aliyeingia madarakani katika
mapinduzi yasiyokuwa na umwagaji damu Oktoba 1999, aliachia madaraka ya urais Agosti
2008, miezi sita baada ya waitifaki na washirika wake kushindwa katika uchaguzi
wa bunge wa Februari 2008 na serikali mpya kutishia kumuangusha. Mwaka mmoja
baadaye akaondoka nchini na kukimbilia nje ya nchi.
Mwezi Machi 2013, Musharraf alirejea Pakistan baada ya
takriban miaka minne ya kukaa uhamishoni mjini London na Dubai kwa leo la
kugombea katika uchaguzi wa bunge uliofanyika mwezi Mei. Lakini alizuiliwa
kugombea kutokana na mashitaka na tuhuma mbalimbali zinazomkabili kutokana na makosa
aliyoyafanya wakati wa utawala wake.
0 comments:
Post a Comment