IDADI ya vifo katika mapambano baina ya wafuasi wa rais zamani wa Misri Muhammad Mursi na vikosi vya polisi imeongezeka na kufikia 51
huku ghasia zikiongezeka na kuhanikiza katika taifa hilo la kaskazini mwa
Afrika.
Wafuasi wa Mursi, aliyeondolewa madarakani kwa mapinduzi
ya jeshi mwezi Julai mwaka huu, walikuwa wakijaribu kukusanyika katika uwanja
mashuhuri mjini Cairo wa Tahrir ambapo polisi walikabiliana nao.
Kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa wizara ya Afya, Ahmed
al-Ansari, kwa uchache watu 45 walipoteza maisha mjini Cairo na wengine kadahaa
kufariki katika eneo la kusini la mji huo.
Afisa huyo aliongeza kuwa vifo vingi vilisababishwa na risasi
na mabomu, wakati polisi walipokuwa wakijaribu kuwatawanya waandamanaji
katikati ya mji wa Cairo.
Aidha, wapatao 270 waliripotewa kujeruhiwa katika ghasia
zilizoyakumba maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri
ilisema kuwa polisi waliwakamata waandamanaji 423 ktaika mji huo.
Wakati huo huo, muungano wa vyama vinavyopinga mapinduzi
ya kijeshi, unaojumuisha chama cha Mursi cha Udugu wa Kiislamu, umeitisha
maandamano zaidi wiki hii na kuwataka wanafunzi katika shule na vyuo vyote kuandamana
kesho Jumanne kupinga kile walichokiita “mauaji yanayoendelea.”
“Muungano wetu unazitupia mamlaka za mapinduzi serikali
iliyoteuliwa na jeshi lawama zote za uwamgaji damu ya Wamisri iliyomwaga leo na
kwa kila Mmisri aliyeuawa leo,” ilisema taarifa ya muungano huo.
Siku ya Ijumaa, maelfu ya wanaharakati wa chama cha
Udugu wa Kiislamu na wafuasi wao walifanya maandamano mjini Cairo baada ya
swala ya Ijumaa kupinga ukandamizaji wa jeshi la Misri.
Gari la jeshi liliwafyatulia waandamanaji risasi za moto
walipojaribu kuingia Uwanja wa Tahrir. Polisi pia walifyatua vitoa machozi katika
harakati za kuwarudisha nyuma.
Misri imekuwa katika hali ya taharuki tangu Julai 3,
baada ya jeshi kumuondoa madarakani Mursi, kusimamisha matumizi ya katiba na
kulivunja bunge. Jeshi hilo pia lilimteua mkuu wa Mahakama Kuu ya Kikatiba,
Adly Mahmoud Mansoour kuwa rais wa mpito.
Serikali ya Mansour ilianzisha operesheni ya kuwadhibiti
wafuasi wa Mursi na kuwakamata zaidi ya wafuasi 2,000 wa chama cha Udugu wa
Kiislamu, akiwemo kiongozi wa chama hicho, Muhammad Badie, aliyekamatwa Agosti
20.
Watu wapatao 1,000 waliuawa ndani ya wiki moja kutokana
na makabiliano baina ya wafuasi wa Mursi
na vikosi vya usalama baada ya polisi kuzivunjilia mbali kambi za waaandamanaji
katika operesheni kubwa Agosti 14.
Mauaji hayo yaliibua lawama za jumuiya ya kimataifa na
kuzifanya taasisi za Kimataifa kutaka ufanyike uchunguzi huru juu ya ghasia
hizo.
0 comments:
Post a Comment