video ikiwaonesha washambuliaji ndani ya jengo la westgate |
POLISI nchini Kenya wamesema kuwa watu walioshambulia
jumba la biashara la Westgate mjini Nairobi walikuwa kati ya wanne na sita,
ikiwa ni idadi ndogo zaidi ya ile iliyoelezwa awali.
Video mpya ya kamera zilzokuwa katika jengo hilo
zinawaonesha washambuliaji hao wakiranda randa na bunduki aina ya AK-47
mikononi mwao
Aidha, jeshi la Kenya liliwataja watu wanne wanaoaminika
kufanya shambulizi hilo. Watu hao ni: Abu Baara al-Sudani, Omar Nabhan, Khattab
al-Kene na Umayr.
Awali Kenya ilikuwa imesema kuwa watu waliohusika na
mzingiro huo uliodumu kwa saa 80 ni baina ya 10 na 15.
"Taarifa tulizonazo sasa kutokana na uchunguzi
wetu, idadi ya washambuliaji ilikuwa kati ya nne na sita,” mkuu wa polisi
nchini humo David Kimaiyo alikiambia kituo cha televisheni cha KTN.
"Hakuna hata mmoja aliyeweza kutoka ndani ya jengo
baada ya shambulizi,” alisema, akimaanisha kuwa watu hao waliuawa katika
mapambano.
Video mpya zilizonaswa na kamera za CCTV kutoka eneo
moja la jengo hilo zinawaonesha wanaume wanne wenye silaha wakizunguka na
kuzurura ndani ya jengo, ikionekana kana kwamba wanawatafuta waathirika wapya.
Juzi Jumamosi Kimaiyo alithibitisha kwamba mwanamke mwenye
asili ya Uingereza, anayejulikana kama “Mjane Mweupe”, Samantha Lewthwaite – ambaye
alidaiwa kuwa mmoja wa washambuliaji – hakuwa miongoni mwao.
"Kuhusu Samantha tumethibitisha kuwa hakuwa sehemu
ya washambuliaji waliokuwa katika jengo,” alisema.
UKATILI
Hapo awali maafisa wa Kenya walikuwa wamedai kuwa
waliwaua washambualiaji watano, lakini video hiyo iliyochukuliwa saa tano za
mzingiro huo uliodumu kwa saa 80, inawaonesha watu wanne tu.
Jambo lililowazi ni kuwa watu hao walikuwa wamejipanga,
na walionekana kutokuwa na wasiwasi wowote na walionakana kuwa na ukatili wa
hali ya juu.
Kamera za usalama zinawaonesha wakiwa kwenye chumba cha
mikate cha ‘supermarket’ saa kadhaa baada ya mzingiro kuanza, ikionekana kuwa
wengi katka wale waliowateka walikuwa wameshakufa.
Wakati mwingine, mmoja wa washambuliaji alisogea kwenye
meza na kukibamiza kioo cha kompyuta.
Wakati huo huo, anaonekana akizungumza na simu,
ikionekana kuwa yumkini alikuwa akifanya mawasiliano na washambuliaji wengine
ndani ya jengo au akiwasiliana na makamanda waliokuwa nje au waliokuwa Somalia.
Adiha, hivi karibuni kikosi maalumu cha jeshi kutoka nje
ya Somalia kiliishambulia ngome moja ya Al-Shabaab katika mji wa Baraawe nchini
Somalia, katika operesheni iliyomlenga kamanda mmoja mwandamizi wa kundi hilo. Al-Shabaab
wanasema kuwa walikabiliana na kikosi hicho na kwamba shambulizi hilo lilifeli.
Marekani ilithibitisha kuwa makomandoo wa jeshi lake la
maji walifanya shambulizi hilo katika taarifa iliyotolewa na wizara ya ulinzi
ya nchi hiyo.
VIDEO YA WESTGATE INAPATIKANA KATIKA UKURASA WETU WA
FACEBOOK WA MZIZIMA 24.
0 comments:
Post a Comment