TAARIFA YA NAIBU WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA
MICHEZO, MH. AMOS MAKALLA KWA VYOMBO VYA HABARI
Napenda kuufahamisha umma kwamba mimi ndiye NILIYERUHUSU
Gazeti la Mwananchi kuendelea na utoaji wa taarifa/habari kwenye tovuti yake,
pia Gazeti la Rai kutoka kila siku.
Ninalazimika kutoa ufafanuzi kwa njia ya maandishi
kutokana na kupigiwa simu nyingi na waandishi wa habari kuhusiana na tamko
jipya la Mkurugenzi wa Habari – Maelezo, Ndg Assah Mwambene kuhoji uhalali wa
Gazeti la Mwananchi kuwa online na Gazeti la Rai kutoka kila siku, badala ya
mara moja kwa wiki (Alhamisi).
Tarehe 4/10/2013 nilifanya mazungumzo na viongozi wa
Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL) na New Habari Corporation (2006)
Ltd kwa upande mmoja na msajili wa magazeti kwa upande mwingine.
Katika kikao hicho cha pamoja na viongozi wa Magazeti ya
Mwananchi na Mtanzania maombi matatu yaliwasilishwa;
1. Ombi la kumuomba waziri apitie upya adhabu
iliyotolewa kwa magazeti hayo. Katika hili Majibu yangu niliwaambia kwamba
mwenye mamlaka juu ya suala hilo ni waziri mwenye dhamana na masuala ya habari
pekee.
2. Ombi la Gazeti la Mwananchi kuwa online na Gazeti la
Rai kutoka kila siku badala ya kutoka siku ya Alhamis.
2.1 New Habari walieleza kuwa siku zilizopita waliwahi
kuomba kwa maandishi (barua) kwamba gazeti la Rai litoke kila siku. Maelezo ya
Naibu Msajili wa Magazeti katika kikao hicho yalikuwa kwamba, kulikuwa na
tatizo la kiufundi katika kurejea maombi hayo na akakiri kuwa hakuna
kinachozuia gazeti la Rai kutoka kila siku. Kutokana na maelezo hayo mimi
niliridhia gazeti hilo sasa liruhusiwe kutoka kila siku.
2.2 Kuhusu gazeti la Mwananchi kuwa online, Naibu
Msajili alisema hakuna sheria yeyote inayoweza kuzuia gazeti hilo kuwa online
ila aliwataka lisionekane gazeti zima kama lilivyo pia
wabadili nembo (Master Head) kwamba waweke nembo ya MCL na siyo ya gazeti
husika ambalo limefungiwa. Pia baada ya maelezo hayo niliridhia gazeti hilo
liwe mtandaoni kwa kuzingatia angalizo lililotolewa na Naibu Msajili wa
Magazeti.
3. Hoja ya tatu ilikuwa ni ile ya Serikali kupitia Idara
ya Habari - Maelezo kuwa na uhusiano mzuri na vyombo vya habari, ili kuepuka
misuguano isiyo ya lazima.
3.1 Pendekezo hili nililipokea na niliwasilisha kwa Mhe
Waziri wa Habari kwa hatua zaidi, likiwamo suala la kupitia upya adhabu na
ushauri wa kujenga uhisiano na vyombo vya habari.
3.2 Masuala ya Gazeti la Mwananchi kuwa online na Rai
kutoka kila siku, NILILITOLEA UAMUZI siku hiyo hiyo, na uamuzi ni kwamba
niliwaruhusu baada ya kuridhika kwamba hakukuwa na ukiukwaji wa sheria yoyote
uliofanywa na waombaji.
Nimeamua kuweka sawa jambo hili kutokana na taarifa ya
Mkurugenzi wa Maelezo ambayo ninaamini kwamba kutolewa na kusambazwa kwake ni
kukosekana kwa mawasiliano kati yake kwa uipande mmoja na Mhe. Waziri, Naibu waziri
na Naibu Msajili wa Magazeti kwa upande mwingine.
Hivyo aliyeruhusu Gazeti la Mwananchi kuwa online na Rai
ni mimi na ndiyo maana kuanzia tarehe 5/10/2013 Gazeti la Rai lilianza kuchapwa
kila siku na kusambazwa, na Gazeti la Mwananchi likaanza kuwa mtandaoni kwa
kuzingatia maelekezo ya Naibu Msajili wa Magazeti.
Imetolewa na:
Amos G. Makalla
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
11 Oktoba 2013
0 comments:
Post a Comment