Uingereza imeahidi kuwa itashirikiana na Zanzibar katika
kuwajengea uwezo wananchi katika sekta ya mafuta na gesi asilia.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania bibi Dianna Melrose,
ameeleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim
Seif Sharif Hamad, nyumbani kwake Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Balozi Melrose amesema anaamini kuwa Zanzibar ina
utajiri mkubwa wa maliasili ikiwemo gesi asilia, na kwamba ili wananchi waweze
kunufaika nayo, ni lazima wawe weledi na wataalamu wazalendo katika fani hiyo.
Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif
Sharif Hamad, amemuhakikishi balozi huyo kuwa Zanzibar itashirikiana na
Uingereza, na kwamba itafarijika kupata msaada huo wa kitaaluma.
Amesema Zanzibar inahitaji sana wananchi wake kupatiwa
taaluma na kujengewa uwezo katika sekta ya mafuta na gesi asilia, haa wakati
huu ambapo suala hilo linatarajiwa kutolewa katika orodha ya mambo ya Muungano.
Mazungumzo hayo pia yalimuhusisha Mkuu wa Idara ya
Afrika Mashariki na Magharibi, Ofisi ya Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola wa
Uingereza bibi Harriet Mathews.
Wakati huo Maalim Seif amekutana na Balozi wa Norway
nchini Tanzania bibi Ingunn Klepsvik na kujadiliana juu ya mambo kadhaa
yakiwemo Serikali ya Umoja wa Kitaifa na mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Amesema viongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa
wanaendelea kushirikiana vizuri katika kutekeleza majukumu ya serikali,
ingawaje bado zipo changamoto katika ngazi za chini za uongozi.
Amesema baadhi ya viongozi wa ngazi za chini wakiwemo
masheha, bado wanahitaji taaluma zaidi katika kuufahamu muundo huo mpya wa
serikali, ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali hiyo, ikiwa ni pamoja na
kuwanganisha wananchi.
Kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba, Maalim Seif
amesema kwa sasa wananchi wanasubiri busara za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye aliyeasisi mchakato huo.
Kwa upande wake balozi Ingunn ameelezea matumaini yake
kuwa mchakato wa katiba mpya utamalizika salama na Tanzania itasonga mbele
kimaendeleo.
Hata hivyo amesema ipo haja kwa Tanzania kusimamia vyema
zoezi hilo, ili kuhakikisha kuwa inapata Katiba itakayokidhi haja, kulingana na
mabadiliko ya hali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.
0 comments:
Post a Comment