VIKOSI maalumu vya kimataifa nchini Somalia vimefanya
shambulizi leo afajiri dhidi ya ngome moja ya al-Shabaab katika mji wa Barawe
uliopo kusini mwa nchi hiyo na kumuua mpiganaji mmoja.
Mji huo unadhibitiwa
na wapiganaji wa al-Shabaab ambao walithibitisha kutokea kwa shambulizi hilo na
kusema kuwa lilishindwa kufanikiwa.
"Wamagharibi wakiwa katika boti walishambulia ngome
yetu kwenye ufukwe wa Barawe na mtu mmoja aliuawa,” alisema Sheikh Abdil Aziz Abu
Musab, msemaji wa operesheni za kijeshi wa al Shabaab wakati akizungumza kwa
njia ya simu na shirika la habari la Reuters.
Nao wakazi wa Barawe walieleza kuwa milio ya silaha
nzito ilisikika kabla ya sala ya alfajiri.
“Niliamka nikasikia sauti ya helikopta, kisha dakika kadhaa
baadaye nikasikia mapigano, milio ya risasi ikahanikiza kwa muda wa kama dakika
10-15,” alisema mkazi mmoja wa eneo hilo.
Shambulizi hilo limekuja wiki mbili baada ya wapiganaji
wa al-Shabab kudai kuhusika na shambulizi katika kituo kimoja cha biashara
mjini Nairobi, ambalo lilisababisha vifo vya watu wasiopungua 67 na wengine
wengi kujeruhiwa.
Serikali mjini Mogadishu imekuwa ikipambana na al-Shabab
kwa miaka sita sasa na kusaidiwa na askari 17,000 wa Umoja wa Afrika kutoka
nchi mbalimbali kama vile Uganda, Burundi, Kenya, na Djibouti.
Somalia haikuwa na serikali imara kuanzia mwaka 1991
mpaka 2012. Mwezi Septemba 2012, wabunge walimchagua kwa kura nyingi Hassan
Sheikh Mohamud kuwa rais mpya wa nchi hiyo.
0 comments:
Post a Comment