MAAFISA nchini Ufilipino wanasema kuwa kwa uchache watu 93
wamethibitika kufariki dunia na makumi kadhaa kujeruhiwa na tetemeko la ardhi
lililopiga katika maeneo ya katikati mwa nchi hiyo inayopatikana kusini
mashariki mwa bara la Asia.
Kitovu cha tetemeko hilo lenye ukubwa wa 7.2 kilikuwa maili 385
(kilometa 619) kusini mashariki mwa Manila, karibu na mji wa Catigbian, na kina
chake kilikuwa maili 12 (kilometa 20).
Kwa mujibu wa Ofisi ya Usalama wa Raia, mamia ya watu
walijeruhiwa wakati tetemeko hilo lilipobomoa majengo na nyumba kadhaa, na
barabara zilibomolewa vibaya sana katika kisiwa cha Bohol na kisiwa cha jirani
cha Cebu.
Minara na majengo ndani na nje ya mji huo wa kitalii
viliharibiwa vibaya sana wakati wa tukio hilo.
Majeruhi walipelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu, lakini
idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka kwa sababu baadhi ya majeruhi wanasemekana
kuwa katika hali mbaya.
Tetemeko hilo lilitokea leo wakati ofisi na shule zikiwa
zimefungwa kwa ajili ya sikukuu ya kitaifa na hilo linaweza kuwa limepunguza
maafa zaidi.
Tetemeko hilo lilifuatiwa na matetemeko kadhaa madogo madogo
yaliyopiga kwenye kina cha kilometa 56.
Ufilipino ni miongoni mwa nchi ambazo zipo katika eneo tete
linalokumbwa na matetemeko ya mara kwa mara kutokana na maumbile ya kijiolojia
yanayoshuhudia harakati mbalimbali za kivolkano.
Mwezi Februari 2012, zaidi ya watu mia moja walifariki dunia na
wengine kupotea baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.9 kukipiga kisiwa
cha Negros, kilometa 100 kutoka eneo kitovu cha tetemeko la leo.
Mwaka 1976, tetemeko lenye ukubwa wa 7.9 lilipiga katika Ghuba
ya Moro kwenye kisiwa cha kusini cha Mindanao, kikaua kati ya watu 5,000 na 8,000.
0 comments:
Post a Comment