TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA UTI WA MGONGO
UTANGULIZI
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa
kwa umma juu ya kuwepo kwa Ugonjwa wa Homa ya Uti wa Mgongo mkoani Rukwa.
Ugonjwa umedhibitika kuwepo baada ya Vipimo vya Maabara
kuonyesha uwepo wa vijidudu vya homa ya uti wa mgongo kwenye sampuli za
wagonjwa waliolazwa kwenye Hospitali ya Mkoa Sumbawanga.
Hadi kufikia tarehe 08/10/2013 jumla ya wagonjwa 21
wameripotiwa katika hospitali ya Mkoa na kati yao wanne (4) wamefariki dunia Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi
wote,
katika mikoa yote ya Tanzania hususani mikoa iliyo
mpakani na mkoa wa Rukwa na vile vile wasafiri wanaotarajiwa kwenda mkoani
Rukwa.
HOMA YA UTI WA MGONGO
Homa ya Uti wa Mgongo inasababishwa na bakteria aitwaye
Neisseria meningitidis. Bakteria huyu ndiye anayeleta milipuko mikubwa ya Homa
ya Uti wa mgongo. Ugonjwa huu hatari unaathiri zaidi meninji na husababisha
athari kubwa kwa ubongo. Ugonjwa huu unapatikana kwa binadamu tu.
Asilimia 50 za wagonjwa hupoteza maisha iwapo matibabu
hayataanzishwa mapema.
Dalili kuu ni Kukakamaa kwa shingo, Homa kali,
Kutokupenda mwanga mkali, Kuchanganyikiwa, Kichwa kuuma pamoja na Kutapika.
Ugonjwa huu unaweza kuathiri ubongo na kupelekea kupoteza uwezo wa kusikia au
kupoteza kabisa uwezo wa kuelewa na kunyambulisha vitu mbalimbali. Iwapo ugonjwa
huu utaathiri ubongo na meninje kwa kiasi kikubwa, umauti hutokea. Dalili za
ugonjwa ni kati ya siku 2 hadi 10 baada ya kupata maambukizi.
Ugonjwa huu unaenezwa kutoka kwa binadamu kwenda kwa
binadamu kwa njia ya hewa au kwa kugusa majimaji/mate kutoka kwa mtu ambaye
tayari ni mgonjwa. Ugonjwa huu unaenea kutoka mtu mmoja hadi mtu mwingine kwa
urahisi na kwa kasi sana iwapo mtu atakuwa karibu na mgonjwa mwenye maambukizi
kwa muda mrefu.
Uambukizo unaweza kutokana iwapo mgonjwa atapiga chafya
au mate ya mgonjwa huyu kuguswa.
Aidha kasi ya maambukizi pia inatokea iwapo mtu ataishi
kwa karibu ndani ya nyumba moja na mgonjwa na kushirikiana naye kwa kula
chakula kwenye chombo kimoja.
Ugonjwa huu unatibika iwapo mgonjwa atawahi hospitalini
na kupewa dawa.
HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA WIZARA
Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa
Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara hususan mikoa
inayopakana na Rukwa. Aidha taarifa hii pia imewakumbusha waganga wakuu warejee
miongozo yao ya kudhibiti Ugonjwa wa Homa ya Uti wa Mgongo yaani namna ya utambuzi
wa mgongwa na, uchukuaji wa sampuli.
Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa
Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipakani.
Kutuma Timu ya Taifa ya Maafa ambayo imeenda kuungana na
timu za Mkoa na Wilaya za Rukwa katika kukabilana na ugonjwa huu ambapo timu
hiyo imeondoka tarehe 10.10.2013.
Kutuma chanjo pamoja na dawa na vifaa Kinga kwa mkoa wa
Rukwa ili kuweza kukabilana na ugonjwa huu.
Elimu ya Afya inaendelea kutolewa katika maeneo ambayo
yamekumbwa na mlipuko na pia mashuleni, vyuoni, magerezani, nakwenye
mikusanyiko na msongamano wa watu. Aidha wananchi wanashauriwa kujenga nyumba
bora zenye madirisha yanayoingiza hewa na mwanga wa kutosha.
Kufungua kambi maalamu mkoani Rukwa kwa ajili ya
wagonjwa wa Homa ya Uti wa Mgongo.
Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa pindi kutoa taarifa
kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa yeyote
atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Wadau wengine
wanaendelea na mikakati ya kuhakikisha ugonjwa huu unathibiwa mkoani Rukwa na
kwa mikoa mengine.
Imetolewa na:
Nsachris Mwamwaja
Msemaji
12 Oktoba 2013
0 comments:
Post a Comment