Tunguli |
KAMPENI ya kitaifa ya kuwaondoa wahamiaji haramu nchini
iliyopewa jina la “Operesheni Kimbunga”, imezidi kuibua mambo mazito baada ya
mganga wa kienyeji kugundulika akitumia uchawi ili kuwalinda wahamiaji hao wasikamatwe.
Mganga huyo aliyefahamika kwa jina la Bahalaye Gwenda
(60), ameifanya kazi hiyo tangu kuanza kwa operesheni hiyo kwa kuwalipisha
wahamiaji haramu sh. 200,000 (laki mbili) kila mmoja wasiweze kukamatwa na
vyombo vya dola vinavyofanya kazi hiyo.
Tukio hilo la kustaajabisha limetokea katika eneo la
Kigaga, Wilaya ya Kibondo, mkoani Kigoma ambapo mganga huyo hutumia hirizi
ambazo ndani yake kuna dawa za kienyeji na vyura wanaopumua kuwauzia wahamiaji
hao.
Taarifa za mganga huyo ziliifikia Kamati ya Ulinzi na
Usalama wilayani humo ambapo Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo,
Bw. Venance Mwamotto, aliongoza kikosi kazi cha wajumbe wa kamati hiyo, polisi
hadi nyumbani kwa mganga.
Kamati hiyo ilipata malalamiko hayo kutoka kwa wahamiaji
ambao walikamatwa licha ya kupewa dawa na mganga huyo ambaye ni raia wan chi jirani
ya Burundi.
Mazingira ya kamati hiyo kufika nyumbani kwa mganga huyo
yalikuwa kama sinema, ambapo wajumbe wa kamati wakiwa na askari polisi, baada
ya kukaribia nyumba yake mganga akiwa ameshika mzizi mkononi na kibuyu
kilichofungwa hirizi, aliwapa ishara ya kutosogelea nyumba hiyo.
“Wakati tukiwa mbele yake tukimfuata, alituambia
tusisogelee nyumba yake kwani uchawi alionao una nguvu kubwa hivyo unaweza
kutudhuru, hatukumsikiliza, tuliendelea kumfuata hivyo alitupa vifaa vyake
chini na kukimbilia ndani.
“Baadhi yetu walikuwa waoga kutokana na sifa za huyu
mganga katika eneo husika wakiogopa kudhurika. Alipoingia ndani alitokea mlango
wa nyuma na kukimbia na sisi baada ya kuingia ndani tulichukua vifaa vyake kama
ushahidi,” alisema Bw. Mwamotto.
Aliongeza kuwa, kikosi kazi alichokiongoza kiliamua
kwenda nyumbani kwa mganga huyo kwa lengo la kumkamata kutokana na malalamiko
waliyoyapata kutoka kwa wateja wake ambao walidai kutumia fedha nyingi kumpa
mtaalamu huyo hivyo walitaka kurudishiwa fedha zao.
Alisema baada ya kuzipasua hirizi walizozikuta, vibuyu
na pembe, walikuta dawa za kienyeji pamoja na vyura wazima wanaopumua. Vitu vingine
walivyovikuta ni vitambaa vyeusi, vyeupe, vyekundu na vitu vingine vya ajabu.
Akizungumzia operesheni hiyo wilayani humo, alisema
wamefanikiwa kukamata sare za Jeshi la Burundi na Kofia vilivyokuwa vikitumika
katika matukio mbalimbali ya uhalifu na wahamiaji haramu.
“Tunaendelea na operesheni yetu kwa kushirikiana na
viongozi ili kuhakikisha wahamiaji wote haramu wanarejeshwa nchini mwao tuweze
kurejesha amani na usalama,” alisema.
Awali Mkuu wa Mkoa huo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, Issa Machibya, alisema wahamiaji haramu wengi
walikuwa wakijihusisha na matukio ya ujangili na biashara ya silaha zikiwemo za
kivita.
Alisema mkoa huo pekee umekamata wahamiaji haramu 4,365
kutoka nchini Burundi katika awamu ya kwanza ya operesheni iliyosambaa katika
mikoa mbalimbali nchini na kuwataka wakazi wa Kigoma kushiriki kikamilifu
katika vita hiyo.
Kwa mujibu wa kiongozi wa timu ya Habari na Mwasiliano
wa Operesheni Kimbunga, Zamaradi Kawawa, alisema katika operesheni hiyo awamu
ya pili iliyofanyika mikoa ya Geita, Kigoma na Kagera, bunduki moja aina ya
SMG, bastola moja, magobole 17 na risasi 115 zikiwemo za bunduki za aina ya SMG
102 na 13 za bastola vilikamatwa.
Wahamiaji haramu waliokamatwa wengi wao ni kutoka nchi
za Burundi ambapo raia wake 114 walikamatwa wakiishi nchini kinyume na sheria
na raia 20 wa Rwamda ambao nao walikamatwa katika kipindi hicho.
CHANZO: Majira
0 comments:
Post a Comment