Hatimaye Uturuki imeondoa marufuku ya kuvaa ushungi kwa
wafanyakazi wa sekta ya umma kama sehemu ya mabadiliko yaliyofanywa na Waziri
Mkuu, Recep Tayyip Erdogan katika
kuboresha demokrasia katika taifa hilo.
Hatua hiyo, ambayo haitazihusu sekta za mahakama, polisi
au jeshi, imeanza kutekelezwa mara moja baada ya kuchapishwa katika Gazeti
Rasmi la Serikali.
Wiki iliyopita, Erdogan alifanya mabadiliko makubwa ya
ndani mengi yakilenga kuboresha haki za jamii ya Wakurdi wachache, lakini pia alitumia
fursa hiyo kupunguza marufuku nyingi zilizowekwa na mfumo wa kisekula katika
taifa hilo.
Chama cha Erdogan cha Haki na Maendeleo kiliahidi
kuiondoa marufuku ya kuvaa ushungi kilipoingia madarakani mwaka 2002.
Hata hivyo, chama kikuu cha upinzani kiliielezea hatua
hiyo kama “pigo kubwa kwa jamhuri ya kisekula” iliyoundwa na muasisi wa Uturuki
ya sasa, Mustafa Kemal Ataturk, mwaka 1923.
Mwaka 1999, mbunge Merve Kavakci, Mturuki mwenye asili
ya Marekani, alifukuzwa bungeni na kupokonywa uraia wake baada ya kuingia
bungeni akiwa amevaa ushungi wakati wa kuapishwa.
Mwezi Februari 2008, Wabunge wa Uturuki walifanya
mabadiliko kwenye katiba yaliyowaruhusu wanawake wa vyuo vikuu kuvaa ushungi,
kwa hoja kwamba wanawake wasingesoma kama hawataruhusiwa kuvaa ushungi.
Hata hivyo, mwezi Juni 2008, Mahakama ya Katiba
ilifutilia mbali mabadiliko yaliyopendekezwa na bunge.
0 comments:
Post a Comment