MAREKANI imesema kuwa kiongozi wa mtandao wa al-Qaeda nchini
Libya, Abu Anas al-Liby, amekamatwa katika “operesheni dhidi ya ugaidi”
iliyofanywa na makomando wake.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, George Little,
alikaririwa akisema kuwa kiongozi huyo “anashikiliwa na jeshi la Marekani katika
eneo salama nje ya Libya.” Hata hivyo, hakujatolewa ufafanuzi zaidi wa jinsi
zoezi hilo lililovyofanyika.
Kiongozi huyo wa al-Qaeda anatuhumiwa kuhusika kwa kiasi
kikubwa katika milipuko iliyotokea mwaka 1998 katika balozi mbili za Marekani
Jijini Dar es Salaam na Nairobi. Katika milipuko hiyo zaidi ya watu 220 waliripotiwa
kupoteza maisha.
Liby, ambaye pia hujulikana kama Nazih al-Ragye, alikuwa
katika orodha ya watu wanaotafutwa sana na FBI. Marekani ilikuwa imetangaza
kitita cha dola milioni tano kwa mtu atakayetoa taarifa zitakazofanikisha
kukamatwa kwake.
Kukamatwa kwa Liby kunakuja baada ya kikosi maalumu cha makomandoo
wa jeshi la maji la Marekani kuyvamia makazi ya kamanda mmoja wa al-Shabab katika
mji wa pwani wa Baraawe nchini Somalia. Hata hivyo, hawakuweza kumkamata
kamanda huyo.
Msemaji wa operesheni za kijeshi wa Al-Shabab, Abdulaziz
Abu Musab alithibitisha kutokea kwa shambulizi hilo na kusema “operesheni hiyo
iliyofeli ilifanywa na wazungu waliokuja katika boti mbili ndogo kutoka kwenye
meli kubwa iliyoweka nanga baharini…mlinzi mmoja wa al-Shabaab aliuawa, lakini
baadaye tulipata msaada zaidi wa wapiganaji wetu kutoka maeneo mengine na
wazungu hao wakakimbia.”
Itakumbukwa kuwa Al-Shabab walidai kuhusika na
shambulizi baya kwenye jengo la kibiashara la Westgate mjini Nairobi Kenya
Septemba 21, lililowaua watu wasiopungua 67 na kuwajeruhi wengine wengi.
Kiongozi wa al-Shabab, Ahmed Godane alisema kuwa
shambulizi walilolifanya Nairobi lilikuwa la kujibu hatua ya jeshi la Kenya
kulivamia eneo la kusini mwa Somalia mwezi Oktoba mwaka 2011.
0 comments:
Post a Comment