ONGEZEKO kubwa la wahamiaji haramu wilayani Ngara mkoani
Kagera linatokana na Watanzania kuamua kuoa wanawake wa Rwanda kuliko
Watanzania kutokana na kutozwa mahari kidogo na kuvutiwa na uzuri wa wanawake
wa Kinyarwanda, imeelezwa.
Kaika hatua nyingine, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta ameahidi kuwasilisha ombi maalumu kwa Rais Jakaya
Kikwete ili wanawake wa Rwanda waliokuwa wameolewa nchini na kukumbwa na
Operesheni Kimbunga, warejee nchini kuungana na familia zao lakini kwa
kuhalalisha ukaazi wao.
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Constatine Kanyasu aliyekuwa
akisoma taarifa ya utekelezaji wa Operesheni Kimbunga awamu ya kwanza
iliyohusisha mpaka wa Rusumo unaozitenganisha Rwanda na Tanzania, alisema
kumekuwepo na ongezeko kubwa la wanaume wa Tanzania kuoa wanawake wa Rwanda
kutokana na udogo wa mahari na uzuri wa Wanyarwanda.
Alisema hata hivyo pamoja na kupendezewa na vitu hivyo
kwa wanawake wa Kinyarwanda lakini wanaume hao wa Tanzania wanashindwa
kuwalipia wake zao hao ada ya Dola za Marekani 550 (Sh 880,000) zinazotozwa
kila baada ya miaka miwili ili kuhalalisha ukazi wao nchini kutokana na
kutobadili uraia kuwa Watanzania.
“Waziri (Sitta) sababu kubwa wanaoyoitoa wanaume wengi
wilayani hapa (Ngara) kama sababu ya Watanzania wengi kuamua kuwaoa Wanyarwanda
ni kutozwa mahari kidogo sana kuliko ile inayotozwa ili kumuoa mwanamke wa
Tanzania. Inasemekana kuna familia wanapokea hadi kuku, mbuzi au fedha kidogo
ili kuruhusu motto wao kuolewa.
“Kwa vile wanapenda kuwa na wake na kwa vile hawana
uwezo wa kifedha wa kutoa mahari kubwa, uamuzi wanaofikia ni kuoa wanawake wa
Kinyarwanda, lakini kwa kufanya hivyo wanajikuta pia wanashindwa kuwalipia wake
zao ada hiyo ya ukazi na kuwafanya kuishi nchini kinyume cha utaratibu,”
alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Alisema kutokana na hatua hiyo Operesheni Kimbunga
imewakumba wanawake wengi waliokuwa wameolewa nchini, hatua iliyosababisha
kubakiwa kwa watoto wasiokuwa na mama wa kuwalea na inayozorotesha uhusiano wa
kifamilia na mataifa ya Rwanda na Tanzania.
Alisema wakati maofisa wa Serikali wa pande hizo mbili
walikuwa na kawaida ya kukutana kila baada ya miezi mitatu kuzungumzia masuala
mbalimbali ya ushirikiano na usalama, tangu kuanza kwa Operesheni Kimbunga
vikao hivyo havifanyiki.
Akizungumzaia kuondoka kwa wanawake walioacha familia
zao, Waziri Sitta ambaye pia alikiri uzuri wa wanawake Wanyarwanda alisema
atawasilisha pendekezo kwa Rais Kikwete ili waweze kuruhusiwa kurejea nchini na
kufuata taratibu za ukazi halali ili kuweza kulea familia zao.
“Hatuna ubaya na watu wa Rwanda hata chembe na tunaomba
walielewe hilo. Operesheni Kimbunga imewakamata pia Wahindi, Wamalawi, Wachina
na hawa Wamakonde, maana wapo Wamakonde wa Kusini mwa Tanzania lakini wapo
Wamakonde wa Kaskazini mwa Msumbiji, hawa pia wamekumbwa na operesheni hii.
“Ikumbukwe kwamba ni haki ya kila nchi kuendesha
operesheni kuhakiki ukazi wa wahamiaji. Ila kwa sababu ya ujirani mwema na hasa
kwa kuzingatia hili la wanawake kuacha familia zao nitapeleka mapendekezo kwa
Rais tuweze kurekebisha maana tunabanwa pia na mikataba ya kimataifa inayohusu
haki za binadamu na watoto,” alisema Sitta.
Akizungumzia malipo ya Dola 550 kila baada ya miaka miwili
zinazopaswa kulipwa ili kuwezesha mke asiye raia kuishi nchini, Waziri Sitta
alisema ni vizuri kiwango hicho kikaangaliwa upya kutokana na ukweli kwamba
wanaume wengi wanaokimbilia Rwanda kuoa wanakwepa ukubwa wa mahari nchini
Tanzania kwa kutokuwa na uwezo.
“Nadhani kuna umuhimu wa kuangalia upya kiwango hiki,
maana kwa mtu asiye na uwezo kulipa ada hiyo tena kwa Dola ya Kimarekani
kunaweza kuwa ni chanzo cha kukwepa sheria na taratibu za nchi yetu. Lengo si
kuwafukuza wenzetu bali kuwataka wafuate sheria,” alisema.
Akizungumza wahamiaji haramu waliorejeshwa makwao,
Kamanda wa Uhamiaji Rusumo, Samwel Mahilane alisema hadi kufikia Oktoba mosi
mwaka huu, wahamiaji 7,858 walirejea makwao kwa hiari kupitia mpaka wa Rusumo,
huku wahamiaji 2,890 wakirejeshwa kwa nguvu na kufanya jumla ya wahamiaji
waliorejea nchini Rwanda kufikia 10,348.
CHANZO: Habari Leo
0 comments:
Post a Comment