Rais wa Guinea Alpha Conde |
CHAMA tawala nchini Guinea kimeshinda katika uchaguzi wa
bunge uliofanyika Septemba 28.
Tumie ya Uchaguzi nchini humo jana Ijumaa Usiku ilitoa
taarifa na kusema kuwa chama tawala nchini humo cha RPG (Rally of the Guinean
People) kinachoongozwa na Rais Alpha Conde kilishinda viti 53 huku washirika
wao kikishinda viti 7 na hivyo kuzoa viti 60 katika ya viti 114 vya bunge.
Chama cha upinzani cha UFDG, kinachoongozwa na Cellou
Dalein Diallo, kilipata viti 37 na chama cha Waziri mkuu wa zamani Sidya Toure
cha UFR kilishinda viti 10. Viti vilivyobaki vilichukuliwa na vyama vidogo
vidogo.
Wapinzani wameyakataa matokeo hayo na kusema kuwa
yamepikwa ili kukisaidia chama tawala.
"Hatutayatambua matokeo, ambayo hayaendani na kura
za wananchi,” alisema msemaji wa muungano wa upinzani, Sydia Toure, kama
alivyonukuliwa na AFP.
Oktoba 4, wapinzani nchini humo walitoa wito wa
kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi wa bunge kwa madai ya kugubikwa na wizi na
ukiukwaji wa taratibu mbalimbali za uchaguzi.
"Upinzani unataka kubatilishwa kwa matokeo kwa
sababu wizi wa kura ulikuwa mkubwa sana,” vilisema vyama vya upinzani katika
tamko la pamoja.
Vyama hivyo vilimshutumu Conde na chama chake “kuchelewesha
amtoke” ya uchaguzi huo kwa lengo la “kumpa rais ushindi ambao hakustahili.”
"Licha ya maonyo ya mara kwa mara, upinzani
unashuhudia mamlaka na CENI (Tume Huru ya Uchaguzi) wakiendelea kuchapisha
matokeo yasiyoakisi kwa vyoyote uhalisia wa kura,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha, wapinzani waliwataka wafuasi wao kuungana na kuwa
tayari kwa maandamano yatakayofanyika ndani ya siku kadhaa zijazo.
"Iwapo matakwa haya ya kubatilishwa matokeo
hayatazingatiwa, upinzani utalazimika kutumia njia zote halali za kuyapinga
ikiwemo maandamano ya umma,” alisema kiongozi mwingine wa upinzani, Aboubacar
Sylla.
Uchaguzi ulifanyika miezi kadhaa baada ya kuakhirishwa
kufuatia machafuko yaliyoua watu kadhaa.
Mnamo Septemba 23, makabiliano baina ya wapinzani na
polisi yaligharimu maisha ya askari mmoja huku zaidi ya watu 50 kujeruhiwa
katika mji mkuu wa nchi hiyo, Conakry.
Guinea ni miongoni mwa nchi masikini zaidi katika ukanda
wa Afrika Magharibi licha ya kuwa na rasilimali mbalimbali kama vile madini na
kadhalika.
0 comments:
Post a Comment