FAMILIA ya aliyekuwa rais wa Misri, Muhammad Mursi,
inasema kuwa amekataa kufanya mazungumzo na viongozi wa kijeshi wa nchi hiyo.
Inasemekana pia kuwa Mursi ameeleza kuwa hivi punde wale
waliohusika na uhalifu dhidi ya Wamisri watafikishwa kwenye mkondo wa sheria.
Misri imeendelea kukumbwa na ghasia tangu Julai 3, pale
jeshi la nchi hiyo lilipomuondoa Mursi madarakani, likasimamisha matumizi ya
katiba na kulivunja bunge. Vilevile jeshi lilimteua mkuu wa mahakama kuu ya
katiba, Adly Mahmoud Mansour, kuwa kiongozi mpya wa serikali ya mpito.
Ripoti zinasema kuwa mkuu wa jeshi, Jenerali Abdul
Fattah al-Sisi alitaka kukutana na mmoja wa wasaidizi waandamizi wa zamani wa
Mursi Emad Abdul Ghafour. Lakini Emad alikataa kufanya mkutano huo kutokana na
uamuzi uliofikiwa na kundi la Muungano wa Kitaifa wa Vyama vinavyotetea Uhalali
wa Urais wa Mursi na kuipinga serikali iliyowekwa na jeshi.
Hayo yanajiri wakati maandamano ya wafuasi wa Mursi
yakihanikiza nchi nzima licha ya juhudi za mamlaka za serikali ya mpito
kujaribu kuyadhibiti.
Jana Ijumaa mchana wafuasi wa Mursi waliandamana katika
miji mbalimbali ya Cairo, Alexandria, Damietta, na Suez, wakitaka Mursi aachiwe
huru na kurejeshwa mamlakani.
Mursi ameshikiliwa katika eneo lisilojulikana tangu
alipoondolewa madarakani. Anatarajiwa kufikishwa mahakamani Novemba 4 kwa
tuhuma za kuchochea ghasia.
Serikali ya mpito imewakamata zaidi ya wafuasi 2,000 wa
chama cha Udugu wa Kiislamu, akiwemo kiongozi mkuu wa chama hicho, Muhammad
Badie aliyekamatwa Agosti 20.
Watu wapatao 1,000 waliuawa katika wiki ya ghasia baina
ya wafuasi wa Mursi na vikosi vya usalama baada ya polisi kuzivunja kambi za
wafuasi hao katika operesheni kabambe iliyofanyika Agosti 14.
Mauaji hayo yalizusha lawama za kimataifa na kuyafanya
mashirika ya kimataifa kutoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru juu ya ghasia
hizo.
0 comments:
Post a Comment