MAHAKAMA moja nchini Italia imetoa huku kwamba aliyekuwa
Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Silvio Berlusconi, aliyekutwa na kosa la ukwepaji
kod, asishike cheo chochote cha umma kwa muda wa miaka miwili.
Mahakama hiyo ya mjini Milan imetoa hukumu hiyo leo
Jumamosi kama sehemu ya mashitaka dhidi ya kiongozi huyo wa zamani anayeandamwa
na kashifa lukuki.
Hata hivyo, kwa kuwa bilionea huyo ni seneta, uamuzi huo
hautakuwa na athari ya mapema.
Kumuondoa Berlusconi kwenye nafasi yake ya useneta
kutategemea upigaji wa kura katika bunge la seneti, ambalo linatarajiwa kukaa
mwezi Novemba.
Mahakama ya Juu nchini Italia ilimtia hatiani Berlusconi
Agosti 1 kwa kosa la ukwepaji kodi, na ikampa adhabu ya kufanya kazi za jamii
au kutumikia kifungo cha nyumbani, na kuifanya hiyo kuwa hukumu ya kwanza dhidi
yake baada ya kesi kadhaa zilizokuwa zikimuandama kwa takriban miaka 20 ya shughuli
zake za kisiasa.
Mnamo Oktoba 2, Berlusconi alilazimika kuachana na
mpango wa kumuangusha Waziri Mkuu Enrico Letta baada ya wabunge zaidi ya 40 wa
chama chake kusema kuwa watamtupa mkono na badala yake watapiga kura kuunga
mkono serikali ya mseto.
Kura hiyo ya kutokuwa na imani na serikali ya mseto
ilikuja baada ya Berusconi kuwaamuru mawaziri wake watano Septemba 28 wajiuzulu
nyadhifa zao katika mgogoro ulioibuka kuhusu hukumu ya ukwepaji kodi
iliyotolewa dhidi yake.
Waziri mkuu huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 77 kwa
sasa anakata rufaa dhidi ya kesi nyingine kama vile, kufanya ngono na binti
mdogo, matumizi mabaya ya ofisi na uvujishaji wa taarifa za siri za polisi
aliyoufanya ili kuharibu picha ya mpinzani wake kisiasa. Aidha , Berlusconi
anachunguzwa kwa tuhuma za kumpa hongo seneta mmoja ili ajiunge na chama chake
cha mrengo wa kulia cha People of Freedom (PDL).
Berlusconi, aliyekuwa waziri mkuu wa Italia kuanzia
mwaka 1994 mpaka 2011, alijiuzulu mwezi Novemba 2011, baada ya kushutumiwa
kushindwa kuimarisha uchumi wa Italia.
0 comments:
Post a Comment