KUTOKANA na shambulio lililofanywa na kundi la Al
Shabaab walioteka jumba la biashara la Westgate na kuua makumi ya raia nchini
Kenya, serikali ya nchi hiyo inakusudia kufumua Idara ya Usalama wa Taifa
(NIC).
Sababu za serikali kuchukua hatua hiyo ni madai kwamba
imeshindwa kuzuia tukio hilo, huku ikihangaika na watu wadogo wadogo wasio
tishio kwa usalama wa nchi.
Akizungumza katika Bunge lililoitishwa kwa dharura jana
jijini Nairobi, Naibu Rais, William Ruto, alisema washambualiaji hao
wamefanikiwa kufanya unyama huo kwa sababu idara hiyo ilikosa umakini.
Ruto alisema lazima idara hiyo ifumuliwe na kufanyiwa
mabadiliko makubwa. Alieleza mshangao wake wa namna watu hao walivyofanikiwa
kupenya na kufanya mauaji makubwa wakati taifa linatumia fedha nyingi katika
sekta ya usalama.
“Tumekuwa tukitumia fedha nyingi kwa ajili ya vikosi vya
usalama nchini hapa, lakini maofisa wetu wamekuwa hawafanyi kazi ipasavyo,
zaidi ya kubaki wakikimbizana na matatuu ‘daladala’ na mama ntilie,” alisema.
Katika mapambano hayo wapiganaji tisa wa kundi la Al
Shabaab wameuawa, huku askari sita wa jeshi wakipoteza maisha na wengine wanane
wakijeruhiwa. Wabunge wengi walisema tukio hilo limedhihirisha kushindwa kwa
idara hiyo.
Mbunge wa Lagdera, Mohammed Shidiye, alisema: “Nafikiri
kwamba huu ni wakati mwafaka wa kufanya upasuaji wa idara hii ili tuweze kupata
watu wachapakazi.”
Mbunge wa Westland, Tim Wanyonyi, alidai wafanyakazi
wengi wa idara hiyo wamekuwa wakisinzia katika kazi zao na kusababisha kushindwa
kuhakikisha Wakenya wanakuwa salama.
Mashambulizi hayo yanadaiwa kuwahusisha watu wawili
wanaodaiwa kuwa raia wa Marekani wenye umri wa miaka 18 na 19, wakiwa na asili
ya Kisomali, wanaosadikiwa kuishi mjini Minnesota, na mmoja wa Uingereza, anayedaiwa
kuhusika na matukio mengi ya kigaidi.
Shutuma hizo za serikali na wabunge zinatokana na kuwapo
kwa taarifa kwamba, washambualiaji hao wamekuwa wakidai kuwa watazishambulia
nchi zote za Afrika zitakazothubutu kupeleka majeshi yake Somalia kuisaidia
serikali ya nchi hiyo.
Taarifa zinasema waliovamia jengo hilo ni sehemu ya wanamgambo
hao, na kwamba huenda ndio waliohusika na mashambulizi kadhaa yaliyotokea
katika nchi ya Uganda miaka kadhaa iliyopita.
Shambulio la juzi katika jengo la Westgate mjini Nairobi
limegharimu roho za zaidi ya watu 62 kutoka mataifa mbalimbali, huku watu
wengine zaidi ya 170 wakijeuhiwa na wengine zaidi ya 50 wakiwa hawajulikani
waliko.
Kundi hilo linadaiwa kufanya shambulio hilo kulipa
kisasi dhidi ya Kenya kutokana na uamuzi wa nchi hiyo kupeleka jeshi lake
Somalia mwaka 2011 kuwafurusha wapiganaji hao wa Al Shabaab waliokuwa
wakishikilia sehemu kubwa ya nchi hiyo.
Katika shambulio la nchini Uganda, kundi la Al Shabaab
lenye mafungamano na Al-Qaeda lilidai kufanya shambulio la mabomu mawili ya
kujitoa mhanga mjini Kampala na kuua watu 74 waliokuwa wakiangalia mechi ya
mpira wa miguu ya Kombe la Dunia, Julai 2010.
Wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema kuwa kundi
hilo linaweza kuishambulia nchi yoyote na wakati wowote, likiona masilahi yake
yanatishiwa.
“Tuliwaonya Uganda wasipeleke majeshi yao Somalia lakini
wakatupuuza. Tuliwaonya kuacha kuwaua watu wetu, na hilo walilipuuza pia.
Mashambulizi ya Kampala yalikuwa ni ujumbe mdogo tu kwao, tutawalenga na
kuwashambulia mahali popote ikiwa Uganda haitaondoa majeshi yake nchini mwetu,”
alisema msemaji wa Al Shabaab, Ali Mahamud Rage.
Rage pia aliionya Burundi kuwa ingekuwa nchi inayofuata
katika mkakati wa mashambulizi wa kundi hilo kutokana na kitendo chake cha
kupeleka majeshi yake nchini Somalia.
Itakumbukwa shambulio la Jumamosi si la kwanza kwa nchi
za Afrika Mashariki. Mwaka 1998 balozi za Marekani hapa nchini na Nairobi, Kenya
zilishambuliwa na al-Qaida na kuua watu
224 raia wa nchi hizi mbili na Wamarekani 12.
Vilevile mwaka 2002, al-Qaida waliishambulia kwa
makombora ndege ya shirika la ndege la Israel na hoteli inayomilikiwa na raia
wa nchi hiyo iliyopo mjini Mombasa.
Kwa muda mrefu wachambuzi wamekuwa na woga kuwa kundi la
al Shabaab lilikuwa likipata nguvu na kugeuka kuwa kitisho cha amani kwa nchi
zote za Afrika Mashariki na za Pembe ya Afrika. Taasisi ya kimataifa ya utafiti
na uzuiaji migogoro ya International Crisis Group iliwahi kusema kuwa:
“Kama ushawishi wa wapiganaji wa nje ukikua na kupata
nguvu ndani ya kundi la al Shabaab, basi mabadiliko ya haraka ya kundi hilo
kuwa tawi kamili la al-Qaida itakuwa haizuiliki tena. Kwamba kundi hilo litasababisha
matatizo makubwa hata nje ya mipaka ya Somalia, na jumuiya ya kimataifa haiwezi
kuchagua kubaki kuwa watazamaji tu.”
Tayari serikali ya Tanzania imesema kuwa imejiimarisha
vema kutokana na tishio hilo, huku Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, Robert
Manumba akidai vikosi vya ulinzi na usalama viko kamili.
CHANZO: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment