Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara, Anatory Choya akiwa amewapigia wananchi magoti kwa maana ya kuonyesha unyenyekevu |
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara, Anatory Choya,
amesema kuwa aliwapigia magoti wananchi wa Kijiji cha Hydom, ili kuonyesha
unyenyekevu kwa wananchi hao aliodai walionekana kujazwa maneno ya uchochezi na
wanasiasa ili wavuruge amani .
Alisema kutokana fujo zilizofanywa na baadhi ya wananchi
hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika majuzi, kwa nafasi yake angeweza
kuagiza hata Jeshi la Polisi kuwadhibiti watu, lakini misingi ya dini yake
haimruhusu kumdhuru mtu zaidi ya kumwonyesha unyenyekevu.
Alisema hali hiyo ndiyo iliyomfanya kuamua kupiga magoti
na kumshtakia Mungu.
“Mimi ni mkristo, unyenyekevu ndiyo nguzo pekee ya
kuonyesha upendo na kudumisha amani. Ningeweza kuagiza polisi wawadhibiti,
lakini sioni sababu kwa kuwa hiyo siyo misingi ya utawala. Ndiyo maana nikaona
bora nitumie njia nyingine ya kumshirikisha Mungu mbele yao,”alisema Choya na
kuongeza:
“Wanasiasa wamekuwa wakipandikiza chuki kwa wananchi kwa
makusudi kwa lengo la kuvuruga amani lakini kwa kumweka Mungu mbele nina imani
tutafanikiwa ili siku moja tusije tukaingia kwenye mkumbo wa Syria na Misri”
Choya alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na
Mwananchi Jumapili, siku chache baada ya kitendo chake cha kupiga magoti mbeye
ya wananchi kwenye mkutano wake wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha
Haydom.
Mkuu huyo wa wilaya alidaiwa pia kuwalaani baadhi ya
wakazi wa Kijiji cha Haydom kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kumdharau na
kutofuata maagizo yake, wakati yeye amewasaidia katika kutatua migogoro
mbalimbali waliyokuwa nayo.
Tukio hilo la kusikitisha lilijitokeza baada ya wananchi
wa kijiji hicho kupinga agizo la Choya, lililowataka kufanya uchaguzi wa kaimu
mwenyekiti wa kijiji hicho, kabla ya kufanya uchaguzi mdogo, ambapo walipinga
kwa kudai kuwa hakuna sheria hiyo.
Mmoja wa wananchi hao alilumbana na mkuu huyo wa wilaya ambapo
Choya alijibu; “Nami nitarudi kwetu." Naye Tikin akasema tena: “Unasema
utarudi kwenu Biharamulo wakati hawakutaki kwani ulifukuzwa ubunge?”
Maneno hayo yalionyesha kumkwaza Choya ambapo alipiga
magoti huku machozi yakimlenga na kumwomba Mungu afanye jambo kwa watu wa Haydom
kwani wanamdharau kabla ya kujitokeza wazee watatu wa Haydom na kumwomba
msamaha mkuu huyo wa wilaya.
0 comments:
Post a Comment