BAADHI ya wakazi wa jijini Dar es Salaam wamefurahia
kuondolewa kwa kikosi cha Polisi Jamii ambacho kiligeuka kuwa kero.
Wakizungumza kwa wakati tofauti jijini Dar es Salaam
jana, wananchi wengi walisema serikali ilikurupuka katika uamuzi wake wa kuunda
kikosi hicho bila maandalizi ya msingi.
Wakiomba majina yao yahifadhiwe, wananchi hao walisema kuwa
hatua ya serikali ya kukiondoa kikosi hicho inadhihirisha namna walivyokosea
tangu awali, ingawa kulikuwa na nia njema.
“Hebu fikiria hao polisi jamii walikuwa ni wezi, vibaka,
watuamiaji wakubwa wa dawa za kulevya na walevi wa pombe haramu ya gongo ambao
hawakupewa mafunzo yaliyostahili. Badala yake walikuwa wala rushwa wakubwa na
mamlaka yao yalizidi yale ya Jeshi la Polisi,” alisema mmoja wa wakazi wa Gongo la Mboto jijini Dar es
Salaam.
“Sijui walitumia vigezo gani kuwapata hao waliojiita Polisi Jamii, maana utakuta
mtu ambaye alikuwa mbabe wa mtaa ndiye amepewa hiyo nafasi, jambo ambalo si
sahihi na hilo liliwafanya wajifanyie kazi kiholela pasipo maadili, maana
walikuwa ovyo ovyo tu,” aliongeza mkazi huyo.
Hata hivyo, alikiri kuwa ingawa baadhi ya sehemu walitoa
msaada mkubwa lakini kwa sehemu kubwa hawakusaidia chochote na ndiyo maana
uhalifu haukwisha, kwani vibaka na wezi wote ni marafiki zao.
Kikosi cha Polisi Jamii kiliondolewa hivi karibuni
kutokana na baadhi ya madereva na wakazi mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam
kulalamikia utendaji kazi wao ambao ulikuwa ukipita mipaka ya Jeshi la Polisi.
CHANZO: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment