WAKATI wananchi wa Afrika Mashariki wakijawa na hofu ya
mashambulio yanayopangwa kufanywa na vikundi vya Al Qaeda na Al Shabab,
imebainika kuna Watanzania waliopewa mafunzo na vikundi hivyo wanaojiandaa
kufanya maovu.
Hayo yamebainika siku chache baada ya wanamgambo wa
kundi la Al Shabab kufanya mashambulio katika Jengo la Biashara la Westgate
mjini Nairobi na kuua watu zaidi ya 70 na kuacha mamia wengine wakiwa
wamejeruhiwa.
Mkuu wa Interpol Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa
Polisi (ACP), Gustav Babile aliyasema hayo jana katika mahojiano maalumu na
MTANZANIA.
Alikuwa akizungumzia kauli ya hivi karibuni iliyotolewa
na Msemaji wa Al Shabab, Sheikh Abdulaziz Abu Muscab aliyetoa tahadhari kwamba
kundi lake linapanga mashambulio mengine Tanzania na Uganda.
Babile alisema taarifa zinaonyesha vijana wa Tanzania waliojiunga
na mafunzo yanayotolewa na vikundi vya
Al Qaeda na Al Shabab, wamefanya hivyo baada ya kushawishiwa watapata utajiri
wa haraka.
Alisema hali hiyo imevifanya vyombo vya ulinzi na
usalama nchini kutoipuuza kauli hiyo ya Sheikh Abdulaziz Abu Muscab.
“Tunajua wapo Watanzania wanapewa dozi za ugaidi, na
sisi siyo kisiwa, watu ni hao hao… tumejipanga kuyakabili haya na kuushirikisha
umma katika ulinzi,” alisema.
Babile alisema kauli ya msemaji wa kundi la Al Shabab ya
kuivamia Tanzania siyo ya kupuuza na kusisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na
usalama nchini viko tayari kukabiliana na lolote litakalotokea.
“Tumeisikia kauli yake kwenye mitandao ya kijamii,
imetufanya kuwa alert (macho) vya kutosha, imetuweka sawa na imetukumbusha kuwa
tunaweza kuvamiwa wakati wowote.
“Hatuja-relax hata kidogo, tumejiweka sawa kwenye human
resources zetu, materials resource na hata frontline officers wetu wako makini
mno.
“Mfano kwenye viwanja vya ndege ambako ni muhimu, kuna
mitambo inayoweza kugundua hati za kusafiria za washukiwa wa uhalifu
wanaotafutwa kimataifa na tutawakamata tu.
“Lakini hata kwenye mipaka yetu yote hatuko peke yetu,
tumepanua wigo wa kupata taarifa za kiintelijensia na katika kufanya kazi hii
tunashirikiana na vyombo vyote vya ulinzi na usalama,” alisema.
Baada ya kufanya mashambulio mjini Nairobi Jumamosi
iliyopita, Msemaji wa Al Shabab, Sheikh Abdulaziz Abu Muscab, aliripotiwa
kwenye mitandao ya kijamii akisema shambulio hilo lilikuwa ni la kulipiza
kisasi baada ya majeshi ya Kenya kuvamia kundi hilo lenye makazi yake mjini
Kismayu, Somalia.
Mitandao ya kijamii pia ilimnukuu Sheikh Abu Muscab
akijigamba kuwa wakati wowote mashambulio ya kikundi hicho yataelekezwa Uganda
na Tanzania.
Wakati huohuo, Babile amesema Mtanzania mmoja alikamatwa
Kenya akishukiwa kuwa ni mmoja magaidi waliovamia jengo la Westgate.
Bila kumtaja jina, alisema mtu huyo ni mkazi wa Arusha
na alikamatwa muda mfupi baada ya kuingia Kenya akitoa Tanzania, akitumia
usafiri wa mabasi ya abiria.
“Walipomkamata wakatuletea taarifa sisi, tukatafuta
kwenye database zetu na information za ndani zikatuonyesha hakuwa mtu hatari,
tukamuachia.
“Kilichowatia hofu na kumshuku mtu huyu ni muda
alioingia Kenya na muda wa tukio lilipotokea… lakini tumeangalia taarifa zote
tukagundua hakuwa na shaka,” alisema Babile.
CHANZO: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment