LWAKATARE AKOSA DHAMANA LEO

Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema Wilfred Lwakatare 



Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura hivi punde wamekwama kupata dhamana baada ya Hakimu anayesikiliza kesi hiyo kutokuwepo mahakamani.

Kesi hiyo hivi sasa inasikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu na hakimu Aloyce Batemana ambaye leo hakuwepo mahakamani.

Awali kesi hiyo ilikuwa katika mahakama hiyo na baadaye kuhamishiwa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam kutokana na masuala ya kisheria, lakini kesi ya Lwakatare na mwenzake ilirejeshwa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu ambako sasa inaendelea.

Hakimu wa Mahakama hiyo, Sundi Fimbo, leo ameahirisha kesi hiyo mpaka Mei 27, mwaka huu baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili.

Awali jopo la mawakili wa Lwakatare walikuwa wamejipanga kumtoa mahabusu baada ya Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam kumfutia mashitaka ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili yeye na mwenzake Ludovick Rwezaura ambayo yalikuwa hana dhamana na kuwaachia shitaka moja la kula njama ambalo sasa lina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kesi hiyo namba 6 ya mwaka 2013, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, imetajwa leo katika mahakama hiyo.

Lwakatare na mwenzake walikuwa wakikabiliwa na mashitaka manne, matatu kati yake yakiwa ya ugaidi na moja la jinai. Mashtaka hayo yalikuwa ya kula njama, kupanga kumteka Dennis Msaki na kisha kumdhuru kwa kutumia sumu, na kufanya mkutano wa vitendo vya kigaidi.

CHANZO: Habari Masai
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment